Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
WALIMU 3,900 WAIMARISHIWA UJUZI KUKIDHI MAHITAJI YA SOKO LA AJIRA

WALIMU 3,900 WAIMARISHIWA UJUZI KUKIDHI MAHITAJI YA SOKO LA AJIRA

 



Matukio Daima Media,Morogoro


Kuimarisha ujuzi wa walimu wa ufundi ni miongoni mwa hatua zinazolenga kupunguza pengo kati ya mafunzo yanayotolewa katika vyuo na mahitaji ya soko la ajira, huku Tanzania ikiendelea kuhitaji wataalamu wenye uwezo wa kufanya kazi kwa vitendo na kuongeza uzalishaji katika sekta mbalimbali za uchumi.


Katika kukabiliana na hitaji hilo, zaidi ya walimu 3,900 wa elimu ya mafunzo ya ufundi na ufundi stadi kote nchini wameanza kupatiwa mafunzo ya mfumo mpya wa umahiri kupitia Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), kwa lengo la kuimarisha ubora wa ufundishaji na ujuzi unaopatikana kwa wanafunzi.


Mafunzo hayo yanatekelezwa kupitia Programu ya Elimu na Ujuzi kwa Ajira zenye Tija Awamu ya Pili (ESPJ II), yakilenga kuwajengea walimu uwezo wa kutumia mbinu za kisasa za ufundishaji na ujifunzaji, ili kuwaandaa wanafunzi kupata ujuzi unaoweza kutumika katika mazingira halisi ya kazi.


Hatua hiyo ina umuhimu katika mazingira ambayo waajiri wanahitaji wafanyakazi wenye uwezo wa kutatua changamoto za kazi, kutumia teknolojia na kuendana na mabadiliko ya uzalishaji, badala ya kutegemea maarifa ya nadharia pekee.


Kaimu Mkuu wa Chuo cha Ualimu wa Ufundi Stadi Morogoro (MVTTC), Dkt Andrew Damian Boi, amesema mafunzo hayo yanawalenga walimu wa vyuo vya ufundi stadi, vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDC) na shule za sekondari zinazotoa elimu ya mkondo wa amali.



Amesema mfumo huo unalenga kuwajengea walimu uwezo wa kuandaa na kuendesha ufundishaji unaozingatia umahiri, ambapo mwanafunzi anatakiwa kuonesha uwezo wa kutumia maarifa na ujuzi alioupata katika mazingira halisi ya kazi.


Kwa upande wake, Mratibu wa Mafunzo ya Muda Mrefu na Muda Mfupi kwa Watumishi wa VETA, Judith Kimaro, amesema mafunzo hayo yanafanyika kwa awamu mbili, ambapo awamu ya kwanza inaendeshwa kwa njia ya mtandao na awamu ya pili itafanyika ana kwa ana.


Ameeleza kuwa matumizi ya teknolojia katika mafunzo hayo yanaongeza uwezekano wa kuwafikia walimu wengi katika maeneo mbalimbali ya nchi, huku akisisitiza umuhimu wa mifumo imara ya TEHAMA na upatikanaji wa intaneti ili kuhakikisha mafunzo yanafanyika kwa ufanisi.


Afisa TEHAMA wa VETA Makao Makuu, Godfrey Pallangyo, ameeleza namna mfumo wa kidijitali unavyowezesha mafunzo hayo na kusaidia walimu kupata maarifa na mbinu zinazohitajika katika utekelezaji wa mfumo mpya wa umahiri.


Amesema matumizi ya mfumo huo yanatarajiwa kuimarisha uwezo wa walimu katika kutumia teknolojia kufundisha, kuandaa mafunzo na kuboresha uwasilishaji wa maarifa kwa wanafunzi.



Mwalimu wa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Don Bosco, Jurieth Shayo, amesema mabadiliko hayo yanaweza kuimarisha ubora wa mafunzo ya ufundi na kuongeza uwezo wa wahitimu kushindana katika soko la ajira, kwa kuwa yanasisitiza zaidi ujuzi wa vitendo na uwezo wa kutumia maarifa katika kazi.


Mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za kuimarisha elimu ya ufundi na ufundi stadi nchini, ili kuongeza upatikanaji wa nguvu kazi yenye ujuzi unaohitajika katika ajira, kujiajiri na shughuli za uzalishaji, huku yakichangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii.




Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3