USHINDANI WAIBUKA BONANZA LA TEF, WANAHABARI MORO, BALILE APONGEZA
Matukio Daima Media, Morogoro
Ushindani mkali uliojitokeza katika bonanza la michezo lililowakutanisha wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini na waandishi wa habari wa Mkoa wa Morogoro umeibua pongezi kutoka kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, aliyesema wenyeji wameonesha uwezo mkubwa na kuwapa wakati mgumu wapinzani wao.
Balile amesema kiwango cha ushindani kilichojitokeza katika michezo hiyo kinaonesha kuwa waandishi wa Morogoro walikuwa wamejiandaa vizuri, hali iliyofanya baadhi ya michezo kuwa na ushindani mkali dhidi ya timu ya TEF.
Katika mpira wa miguu timu ya waandishi wa habari wa Morogoro iliongoza kwa ushindi wa bao 4-0 dhidi ya wahariri wanaounda Jukwaa la wahariri Tanzania TEF.
Ushindani huo pia umethibitishwa na Hafidh Kido kutoka TEF, ambaye ameibuka mshindi katika mchezo wa kukimbia ndani ya gunia, akisema maandalizi yaliyofanywa na waandishi wa Morogoro yalifanya mashindano hayo kuwa magumu.
Ushindani huo pia umethibitishwa na Hafidh Kido kutoka TEF, ambaye ameibuka mshindi katika mchezo wa kukimbia ndani ya gunia, akisema maandalizi yaliyofanywa na waandishi wa Morogoro yalifanya mashindano hayo kuwa magumu.
Hata hivyo, mbali na matokeo ya michezo, Meneja na Mratibu wa TEF Bonanza, Caren-Tausi Mbowe, amesema kuendeleza mashindano ya aina hiyo ni muhimu katika kujenga afya bora, urafiki na mshikamano miongoni mwa wanahabari.
Bonanza hilo lililofanyika mkoani Morogoro kama sehemu ya shughuli za Mkutano wa Tisa wa TEF limewakutanisha wahariri zaidi ya 200 pamoja na waandishi wa habari wa Morogoro, wakishindana katika michezo ya mpira wa miguu, pete, kikapu, bao na kuvuta kamba.
Mratibu wa TEF Bonanza mkoani Morogoro, Idda Mushi, amesema tukio hilo limekuwa na umuhimu wa kipekee kwa kuwa limewapa wanahabari nafasi ya kujumuika, kuonesha vipaji vyao na kushiriki moja kwa moja katika michezo ambayo mara nyingi wamekuwa wakiifuatilia na kuihabarisha jamii kupitia kazi zao za kila siku.



