REA YAWANOA VIONGOZI WA JUMUIYA YA WAZAZI CCM KUHUSU NISHATI SAFI
Matukio daima App Dodoma
Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umeendesha mafunzo maalum kuhusu matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia kwa viongozi wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutoka wilaya zote za Tanzania Bara na Visiwani, ikiwa ni mkakati wa kuwafanya kuwa mabalozi wa mabadiliko katika jamii zao.
Akizungumza katika mkutano maalum wa jumuiya hiyo uliofanyika jijini Dodoma tarehe 28 Novemba, 2026, Mhandisi Miradi kutoka REA, Kelvin Tarimo, amesema serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanahamia kwenye teknolojia za nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
Mhandisi Tarimo amebainisha kuwa safari ya kuleta nishati safi inaenda kwa kasi kupitia miradi mbalimbali. Miradi hiyo ni pamoja na utoaji wa ruzuku ya hadi asilimia 85 kwenye majiko banifu, usambazaji wa mitungi na majiko ya gesi (LPG) ya kilo 15 na sita, pamoja na uwezeshaji wa nishati safi katika taasisi za umma.
Aidha, REA inatekeleza uwezeshaji wa miundombinu ya usambazaji wa gesi asilia kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), sambamba na ujenzi wa viwanda vya mkaa mbadala kwa kushirikiana na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO).
"Zaidi ya majiko 141,000 tayari yametolewa nchi nzima, huku utekelezaji ukivuka asilimia 70 na kunufaisha kaya nyingi. Pia, tunaendelea kufunga miundombinu ya nishati safi katika shule za sekondari, magereza yote Tanzania Bara pamoja na kambi za Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ili kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa," amesema Mhandisi Tarimo.
Ametoa wito kwa viongozi hao wa Jumuiya ya Wazazi kutumia changamoto ya ukosefu wa nishati safi iliyopo kwenye jamii kama fursa ya ushirikiano na uwekezaji, huku akiwasisitiza kuwa mabalozi wa nishati safi kwa wananchi wengine.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa, Comrade Fadhili Maganya, ameishukuru REA kwa mafunzo hayo na kuiomba kuangalia namna ya kuzisaidia shule zinazomilikiwa na jumuiya hiyo ambazo bado zinatumia kuni na mkaa.
"Tutawasilisha maombi maalum REA ili na sisi tuwe miongoni mwa wanufaika wa moja kwa moja wa miradi hii ya nishati safi katika shule zetu," amesema Comrade Maganya.





