MKALAMA: BARAZA LA MADIWANI LAONYA KUINGILIWA MAJUKUMU
Na Elisante John, Singida
Jumamosi, Septemba 5, 2026
Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama mkoani Singida imesema haitakubali majukumu ya Baraza la Madiwani kuingiliwa na mtu yeyote kwa maslahi binafsi, ikisisitiza kuwa itaendelea kutekeleza wajibu wake kwa mujibu wa sheria, taratibu na misingi ya utawala bora.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Mohamed Juma, wakati akihitimisha mkutano wa robo ya nne ya mwaka wa fedha 2025/2026, uliofanyika katika ukumbi wa Halmashauri mjini Nduguti, huku akitaka taasisi hiyo kuheshimiwa katika kutekeleza majukumu yake.
Juma amesema kuwa, Baraza la Madiwani limeanzishwa kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi, likiongozwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo hakuna mtu anayepaswa kulidharau, kulichezea au kuingilia utekelezaji wa majukumu yake.
Amesema alilazimika kutoa ufafanuzi huo baada ya Baraza hilo kukutana kama Kamati kushughulikia tuhuma dhidi ya mmoja wa watumishi wa Halmashauri, anayedaiwa kukiuka misingi na maadili ya utumishi wa umma.
ila kutaja jina la kiongozi anayedaiwa kuingilia shughuli za Halmashauri wala mtumishi anayekabiliwa na tuhuma hizo, Juma aliiagiza Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji kuandika barua kwa haraka kwenda kwa Mkuu wa Mkoa, ili kuomba ridhaa ya kuitisha kikao maalumu cha Baraza la Madiwani kwa ajili ya kushughulikia tofauti zilizojitokeza kati ya pande hizo.
Katika hatua nyingine, Baraza hilo lilimtunuku Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, hajati Asia Messos, tuzo ya pongezi kwa kutambua mchango wake katika kusimamia majukumu ya Halmashauri, kuimarisha utawala bora na kuongeza mapato, hatua iliyosaidia kuchochea utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Baadhi ya madiwani, akiwamo Anthony Kahema wa Nkalakala, Linza John wa Matongo, Salumu Lindi wa Ibaga na Zainabu Kihara wa viti maalumu, waliunga mkono kutolewa kwa tuzo hiyo, wakisema hajati Messos amekuwa akionesha usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo na anastahili kupewa pongezi pamoja na ushirikiano katika kutekeleza majukumu yake.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo, hajati Messos alishindwa kujizuia na kutoa machozi ya furaha, akilishukuru Baraza kwa kutambua mchango wake katika kusimamia shughuli za maendeleo katika Halmashauri hiyo.
Hajati Messos alisema mafanikio hayo hayakuwa yake binafsi, bali ni matokeo ya ushirikiano kati yake na watumishi wenzake, akiwataka kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kusimama pamoja katika kuleta maendeleo.
“Nimepokea tuzo na zawadi hii kwa furaha sana. Kazi hii sikuifanya peke yangu, bali pamoja na watumishi wenzangu wote 1,527 wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama. Wote pokeeni zawadi hii na nawaomba endeleeni kuchapa kazi na tusimame imara ili kuiletea wilaya yetu maendeleo,” alisema hajati Messos.




