CHUO KIKUU IRINGA CHAOMBOLEZA KIFO CHA MHADHIRI SOLANUS NICHOMBE
Sep 2, 2026
NA MATUKIO DAIMA MEDIA, IRINGA
CHUO Kikuu cha Iringa kimeeleza kusikitishwa na kifo cha aliyekuwa mtumishi wake, Solanus Baptisti Nichombe, aliyefariki dunia Agosti 31, 2026, baada ya kuugua kwa muda.
Akisoma taarifa ya Mkuu wa Chuo Kikuu cha Iringa kwa niaba yake, Blandina Kisawike alisema chuo hicho kimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha aliyekuwa mtumishi wake.
Alisema uongozi, wafanyakazi na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Iringa wanatoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wa Marehemu Nichombe.
“Marehemu alikuwa mtumishi wa Chuo Kikuu cha Iringa aliyejitolea kwa uaminifu, uadilifu na bidii katika kutekeleza majukumu yake.
“Katika kipindi chote cha utumishi wake, alionesha weledi mkubwa na moyo wa kulitumikia chuo katika nafasi mbalimbali alizowahi kushikilia,” alisema Kisawike.
Alisema chuo kinatambua na kuthamini mchango wa marehemu katika maendeleo ya taasisi hiyo, pamoja na mahusiano mazuri aliyoyajenga na wafanyakazi wenzake, wanafunzi na wadau aliowahudumia.
Kisawike alisema kifo cha Nichombe kimeacha pengo kubwa katika familia na jumuiya nzima ya Chuo Kikuu cha Iringa.
“Katika kipindi hiki kigumu, chuo kinasimama pamoja na familia ya marehemu na kuwaombea nguvu, faraja na uvumilivu.
“Tunamshukuru Mungu kwa maisha ya marehemu na tunaiombea familia iendelee kuwa na moyo wa subira na tumaini,” alisema.
Chuo Kikuu cha Iringa kimetoa rambirambi na usafiri wa kupeleka mwili wa marehemu mkoani Njombe kwa ajili ya mazishi.
“Mungu ailaze roho ya Marehemu Solanus Baptisti Nichombe mahali pema peponi.
Awali akisoma wasifu wa marehemu, mwanafamilia Pienzia Nichombe alisema Solanus Baptisti Nichombe alizaliwa Aprili 5, 1963, katika Kijiji cha Kifanya, Wilaya ya Njombe mkoani Njombe.
Alisema marehemu alianza elimu ya msingi mwaka 1981, baadaye akajiunga na Shule ya Sekondari Lupago kabla ya kuendelea na masomo katika Shule ya Sekondari ya Biashara Iringa.
Marehemu alihitimu mwaka 1989 na kupata Cheti cha Biashara (CBE) Shinyanga.
Kuanzia mwaka 1989 hadi 1990, alisoma katika Chuo cha Uhasibu Arusha, kabla ya kuendelea na masomo ya Astashahada ya Uhasibu katika Taasisi ya Maendeleo ya Menejimenti (IDM) Mzumbe kuanzia mwaka 1991 hadi 1994.
Pia, alihitimu Shahada ya Uzamili ya Utawala wa Biashara katika Chuo Kikuu cha Mzumbe, Kampasi ya Dar es Salaam, alikosoma kuanzia mwaka 2007 hadi 2009.
Mwaka 2011, alipata sifa ya kitaaluma ya uhasibu ya Certified Public Accountant (CPA).
Katika maisha ya familia, marehemu alifunga ndoa Novemba 14, 1997, katika Kijiji cha Kifanya.
Ameacha mke na watoto watatu, wawili wa kiume na mmoja wa kike.
Safari ya utumishi
Pienzia alisema marehemu alianza kazi yake ya ualimu katika Shule ya Wasichana Iringa, kabla ya kuhamia katika taaluma ya uhasibu.
Kuanzia mwaka 1995 hadi 1997, alifanya kazi katika Kampuni ya Ruaha Bottling. Mwaka 1999, aliendelea na kazi za uhasibu katika Shule ya Sekondari Highland.
Baadaye, kuanzia mwaka 2002 hadi 2003, alifanya kazi ya uhasibu katika Mradi wa MEMA.
Mwaka 2004, marehemu alijiunga na Chuo Kikuu cha Iringa, ambako alihudumu katika nafasi mbalimbali, akianza kama mhasibu na baadaye kuwa Project Accountant.
Kuanzia mwaka 2011 hadi 2014, alihudumu kama Financial Officer na baadaye kukabidhiwa majukumu ya Assistant Chief Financial Officer, nafasi aliyoitumikia kwa uaminifu na uadilifu mkubwa.
Mwaka 2014 hadi 2015, alihudumu kama Project Accountant, akionesha uwezo mkubwa katika utekelezaji wa majukumu ya kihasibu.
Kuanzia Novemba 2015 hadi alipostaafu, Marehemu Nichombe alihudumu kama Assistant Lecturer katika Kitivo cha Biashara na Uchumi cha Chuo Kikuu cha Iringa.
Katika nafasi hiyo, alishiriki kufundisha, kuwajengea wanafunzi maarifa na kutekeleza majukumu mengine ya kitaaluma chuoni hapo.
Ugonjwa na matibabu
Mwanafamilia huyo alisema marehemu alianza kuumwa mwanzoni mwa mwaka 2025 na kwenda katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa, ambako alifanyiwa vipimo na kuendelea kupatiwa matibabu.
Baadaye, alipelekwa katika hospitali mbalimbali kwa uchunguzi na matibabu zaidi, zikiwamo Hospitali ya CCBRT, KCMC, Bugando, Aga Khan, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa, Benjamin Mkapa, DCMC Dodoma na Muhimbili.
Marehemu aliendelea kupatiwa matibabu hadi Agosti 31, 2026, alipofariki dunia akiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa.
Familia imetoa shukrani kwa wauguzi na madaktari wa hospitali zote alizopatiwa matibabu.
Pia, imewashukuru ndugu, jamaa, marafiki na majirani kwa misaada ya hali na mali waliyoitoa wakati wa ugonjwa na msiba.
Mwili wa Nichombe umeagwa leo katika kanisa la RC Parokia ya Mkimbizi Iringa mjini na kusafirishwa kwenda Kijiji cha Kifanya mkoani Njombe kwa mazishi yatakayofanyika Alhamisi Septemba 3/2026
“Mungu alitoa na Mungu ametwaa, jina lake lihimidiwe.
TAZAMA PICHA ZA MATUKIO YOTE CHINI⬇️⬇️⬇️




























































































