Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
RAIS SAMIA AFANYA UTEUZI NA UHAMISHO WA WAKUU WA MIKOA

RAIS SAMIA AFANYA UTEUZI NA UHAMISHO WA WAKUU WA MIKOA

 


NA MATUKIO DAIMA MEDIA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amefanya uteuzi na uhamisho wa Wakuu wa Mikoa pamoja na Makatibu Tawala wa Mikoa katika mabadiliko yaliyotangazwa leo, Agosti 27, 2026.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Bakari S. Machumu, mabadiliko hayo yamehusisha uteuzi wa Wakuu wa Mikoa wanne na uhamisho wa wengine sita.

Katika uteuzi huo, CP. Salum Rashid Hamduni, aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, huku Alexander Pastory Mnyeti akiteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Geita.

Aidha, Stanslaus Haroon Nyongo ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani, wakati Jumanne Abdallah Sagini akiteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya.

Katika uhamisho wa Wakuu wa Mikoa, Martine Reuben Shigela amehamishwa kutoka Geita kwenda Manyara, huku Said Mohamed Mtanda akihamishwa kutoka Mwanza kwenda Simiyu, akichukua nafasi ya Anamringi Macha ambaye amestaafu.

Vilevile, Abubakar Mussa Kunenge amehamishwa kutoka Pwani kwenda kuwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe, akichukua nafasi ya Jabiri Omari Makame ambaye atapangiwa majukumu mengine.

Beno Moris Malisa amehamishwa kutoka Mbeya kwenda kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, akichukua nafasi ya Paul Matiko Chacha ambaye aliteuliwa kuwa Katibu wa NEC – Idara ya Organizesheni ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Naye Adam Kighoma Malima amehamishwa kutoka Morogoro kwenda kuwa Mkuu wa Mkoa wa Lindi, akichukua nafasi ya Zainab Telack ambaye amestaafu, huku Queen Cuthbert Sendiga akihamishwa kutoka Manyara kwenda kuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.

MABADILIKO YA MAKATIBU TAWALA

Katika hatua nyingine, Rais Samia amemteua Richard Marcellino Kayombo kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani.

Pia, Barahindya Mavuganya Elikana amehamishwa kutoka Mwanza kwenda kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya; Dkt. Fatuma Ramadhan Mganga amehamishwa kutoka Singida kwenda Mwanza; Pili Hassan Mnyema amehamishwa kutoka Pwani kwenda Shinyanga; na Rodrick Lazaro Mpogolo amehamishwa kutoka Mbeya kwenda kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida.

Taarifa ya Ikulu imeeleza kuwa uapisho wa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa walioteuliwa utafanyika katika tarehe itakayopangwa baadaye.

Taarifa hiyo imetolewa Dar es Salaam, Agosti 27, 2026.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3