Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
WAZIRI KOMBO AAGANA NA MHE. MASSALA, BALOZI WA DRC NCHINI TANZANIA

WAZIRI KOMBO AAGANA NA MHE. MASSALA, BALOZI WA DRC NCHINI TANZANIA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Mahmoud Thabit Kombo (Mb), amekutana na kuagana na Balozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Mheshimiwa Jean Pierre Massala, ambaye amehitimisha muda wake wa uwakilishi nchini Tanzania.


Mkutano huo umefanyika leo, Septemba 4, 2026, katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje jijini Dar es Salaam.
Katika mkutano huo, Waziri Kombo alimpongeza Balozi Massala kwa mchango wake katika kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano wa pande mbili kati ya Tanzania na DRC, hususan katika maeneo ya maendeleo, biashara na uwekezaji.

Waziri Kombo amesema Tanzania imeazimia kuimarisha zaidi ushirikiano wa kimkakati na DRC katika sekta mbalimbali, zikiwemo uchukuzi, madini, mafuta na gesi, ulinzi na usalama, pamoja na kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya pamoja yenye manufaa kwa wananchi wa nchi hizo mbili.

Miongoni mwa miradi ya kipaumbele ni ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), inayolenga kuunganisha Tanzania na DRC kupitia Burundi, pamoja na ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ya Mawimbi ya Mwanga kutoka Kigoma nchini Tanzania hadi Kalemie, Mkoa wa Tanganyika nchini DRC, kupitia Ziwa Tanganyika.

Aidha, Tanzania na DRC zimekubaliana kuharakisha uanzishwaji wa Tume ya Pamoja ya Kiuchumi (JEC), ambayo inalenga kurahisisha utekelezaji wa miradi ya pamoja na kutengeneza fursa mpya za kiuchumi kwa nchi hizo.

Kwa upande wake, Balozi Massala ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano alioupata katika kipindi chake cha uwakilishi nchini na kusisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano wa kimkakati katika sekta mbalimbali za maendeleo kati ya Tanzania na DRC.



 

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3