*DKT. MWIGULU: KILA KIJIJI KUWA NA SEKONDARI*
Sep 5, 2026
*_▪︎ Aelekeza fedha zinazookolewa kwenye kubana matumizi zielekezwe kwenye huduma za wananchi_*
*_▪︎ Aagiza magari ya kubeba wagonjwa yawe na mafuta, aonya wanaowachangisha wagonjwa_*
*_▪︎ Ampongeza Afisa Elimu aliyesimamia shule kuongoza kitaifa_*
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema Serikali imejipanga kufanya mageuzi makubwa katika sekta ya elimu, ikiwemo kuhakikisha kila kijiji kinakuwa na shule ya sekondari, na zaidi ya vyumba 16,000 vya madarasa vikitarajiwa kujengwa ili kukidhi ongezeko la wanafunzi.
Dkt. Mwigulu amesema hayo leo, Jumamosi, Septemba 05, 2026, wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Bahi, mkoani Dodoma, katika Viwanja vya Halmashauri ya Bahi, alipokuwa katika ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kuwasikiliza wananchi na kushughulikia changamoto zinazowakabili.
Amesema uamuzi wa kuongeza muda wa elimu ya lazima hadi kidato cha nne unaleta mahitaji makubwa ya miundombinu ya elimu, yakiwemo madarasa, maabara na maktaba.
“Tunaposema elimu ya lazima itakuwa mpaka kidato cha nne, maana yake tunasema kila kijiji kiwe na sekondari. Tunaongelea mahitaji ya madarasa zaidi ya vyumba 16,000.”
Waziri Mkuu amesema Serikali haitaki kuona watoto wakirejea katika mazingira ya kusoma chini ya miti, kukosa madarasa au kusoma katika mazingira ya msongamano, akisisitiza kuwa maandalizi ya mapema ni muhimu kukabiliana na mahitaji hayo.
Amesema Serikali pia inahitaji kuongeza idadi ya maabara, akieleza kuwa mahitaji yanaweza kufikia takribani maabara 8,000, pamoja na maktaba, ili kuimarisha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.
Aidha, Dkt. Mwigulu amewataka viongozi wa Serikali kubadili baadhi ya taratibu zinazoweza kuokoa fedha na kuelekeza rasilimali hizo kwenye huduma zinazogusa maisha ya wananchi moja kwa moja.
Amesema viongozi wanapaswa kuweka mbele wajibu wa kuleta maendeleo kuliko kutafuta sifa zinazohusisha gharama zisizo za lazima.
Ametoa mfano wa misafara mikubwa ya viongozi na mikutano inayohusisha idadi kubwa ya watendaji kusafiri kwenda vituo vingine, akisema fedha zinazoweza kuokolewa zinapaswa kuelekezwa katika ujenzi wa madarasa, maabara, madawati na huduma nyingine muhimu.
“Kila tunapoweza kupata akiba tuielekeze kwenye jambo linalogusa maisha ya wananchi wetu ya kila siku.”
Kuhusu huduma za afya, Waziri Mkuu amewataka viongozi kuhakikisha magari ya kubeba wagonjwa ya Serikali yanakuwa na mafuta na wagonjwa wanaohitaji rufaa hawalazimishwi kuchangisha fedha kwa ajili ya mafuta.
Amesema Serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa katika ujenzi wa hospitali, vituo vya afya, ununuzi wa magari ya kubeba wagonjwa, vifaa tiba na ajira za wataalamu, hivyo watendaji wanapaswa kuhakikisha uwekezaji huo unawanufaisha wananchi.
Ameonya kuwa mtumishi anayemlazimisha mgonjwa au ndugu yake kuchangisha fedha kwa ajili ya mafuta ya gari la kubeba wagonjwa anapaswa kuchukuliwa hatua, huku akiwataka wananchi kuripoti watumishi wanaokiuka taratibu na kuwanyima wananchi huduma wanazostahili.
Dkt. Mwigulu pia amempongeza Mkuu wa Divisheni ya Elimu ya Awali na Msingi, Boniface Wilson Mwakasole, kwa utendaji wake katika kuboresha elimu wilayani Bahi, akieleza kuwa amefuatilia kazi yake na kubaini mafanikio yaliyopatikana, ikiwemo Shule ya Msingi Chiona kuongoza kitaifa katika elimu ya msingi.
Amesema watendaji wanaofanya vizuri wanapaswa kutambuliwa na kupewa majukumu makubwa zaidi yanayolingana na uwezo wao.
Akimtolea mfano Boniface Wilson Mwakasole, Waziri Mkuu ameelekeza kuwa endapo mtendaji huyo ataondolewa Bahi, apandishwe cheo na kupewa jukumu kubwa zaidi kutokana na utendaji wake.
“Huyo mtu mzuri wa aina hiyo kama mnataka kumhamisha, mpandisheni; mpeni mkoa kama mnataka kumtoa Bahi. Kama hamjapata mkoa, msimhamishe, mbakizeni hapa hapa. Amefanya kazi nzuri ya kuigwa.”
Amesema utendaji mzuri unapaswa kuwa msingi wa kumpa mtumishi majukumu makubwa, akisisitiza kuwa mtu anayefanya kazi vizuri hahitaji kuomba nafasi kwa kutumia ushawishi kwa sababu kazi yake yenyewe inamtambulisha.
“Mtu anayefanya kazi nzuri wala hahitaji lobbying, hauhitaji kuomba-omba kazi; kazi inakutambulisha.”
Amesema Serikali inapaswa kuwa na utamaduni wa kutambua na kupongeza watendaji wanaofanya vizuri, sambamba na kuchukua hatua kwa wale wanaoshindwa kutimiza wajibu wao.
Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya maendeleo katika Wilaya ya Bahi, ikiwemo miradi ya maji, afya, elimu, umwagiliaji, barabara na madaraja.
Amesema amepokea mahitaji mbalimbali yaliyowasilishwa na viongozi wa wilaya na mkoa na amemtaka Naibu Waziri anayesimamia Serikali za Mitaa kuyafuatilia kwa karibu ili hatua zichukuliwe katika maeneo yenye uhitaji.
Pia ameeleza kuwa maeneo yanayounganisha miji na vijiji, lakini wananchi wake bado wanaishi katika mazingira ya vijijini, yataendelea kunufaika na utaratibu wa kuunganishiwa umeme kwa gharama zinazotumika maeneo ya vijijini.


