Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
BARAZA LA VYAMA LAAPA KUONDOA CHUKI ZA KISIASA

BARAZA LA VYAMA LAAPA KUONDOA CHUKI ZA KISIASA


Na Lilian Kasenene, Morogoro 
Matukio DaimaApp 

Baraza la Vyama vya Siasa Tanzania limesema litahakikisha linafanya kazi ya kuondoa chuki za kisiasa nchini baina ya vyama vya siasa na Serikali, hatua inayolenga kujenga mahusiano mazuri katika jamii na kuendeleza misingi ya demokrasia.

Mwenyekiti wa Baraza hilo, Juma Ali Khatib, alisema hayo mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa kuchagua viongozi wa kamati za Baraza hilo.

Alisema viongozi wapya waliochaguliwa wataendelea kusimamia na kufuata sheria za vyama vya siasa pamoja na sheria za nchi.

Alisema kazi ya Baraza hilo ni kuishauri Serikali na kujenga ukaribu zaidi kati ya Serikali, vyama vya siasa na wananchi, kwa lengo la kuhakikisha masuala yenye maslahi mapana kwa Taifa yanapewa kipaumbele.

“Kubwa zaidi ni kutaka kujenga amani ya nchi yetu. Kuna mambo mengi yamepita baada ya kumaliza uchaguzi na sasa Serikali inakwenda mbele na kazi zinafanyika,” alisema.

Alisema vyama vya siasa vina wajibu wa kushiriki katika kuijenga nchi, kuunganisha Serikali na jamii na kuhakikisha wananchi wanaendelea kufanya shughuli zao za kijamii kwa amani.

“Sisi kama vyama vya siasa, nia yetu ni kuijenga nchi yetu, kuunganisha Serikali na jamii ili waendelee kufanya shughuli zao za kijamii,” alisema.

Alisema vyama vya siasa vitaendelea kutangaza sera na ilani zao kwa maslahi ya Taifa na maendeleo ya baadaye.

Aidha, alisema kamati mpya itahakikisha inaendeleza misingi ya demokrasia na kusimamia sheria zinazotolewa na Msajili wa Vyama vya Siasa, sheria za vyama vyao pamoja na sheria za nchi bila kuleta taharuki.

Alisema hatua hiyo inalenga kuonyesha ukomavu wa kisiasa ndani ya Baraza la Vyama vya Siasa Tanzania, akieleza kuwa kazi hiyo imekuwa ikiwezeshwa na kusimamiwa kwa karibu na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.

“Siku zote Msajili amekuwa mstari wa mbele kukaa na viongozi wa vyama vya siasa Tanzania kwa kuwaelimisha wajibu wetu na namna tunavyoweza kujua wajibu wetu na kuishauri Serikali kama sheria inavyotutaka,” alisema Khatib.

Alisema lengo la Baraza hilo ni kuhakikisha vyama vya siasa vinaendelea kushirikiana na Serikali katika kujenga nchi, kuwaunganisha Watanzania na kufanya kazi kwa bidii kwa kushirikisha wananchi kikamilifu.

Akizungumza katika mkutano huo, Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Mohamed Ali Mohamed, aliwaasa viongozi wa vyama vya siasa pamoja na wanaharakati kutumia lugha za kistaarabu wakati wa kuwasilisha hoja zao.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Masuala ya Uchaguzi ya Baraza la Vyama vya Siasa Tanzania, Majalio Kyara, alisema ni muhimu kuendelea kuimarisha demokrasia nchini ili kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na amani.

Mwisho..


 

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3