Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
TPF NET YATAKIWA KUIJENGA IMANI KWA JAMII

TPF NET YATAKIWA KUIJENGA IMANI KWA JAMII


DODOMA. 

Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma


MTANDAO wa Polisi Wanawake Tanzania (TPF NET) umetakiwa kuongeza ushirikiano na wananchi pamoja na kuendeleza shughuli za kijamii zitakazosaidia kujenga imani na mahusiano bora kati ya Jeshi la Polisi na jamii.


Wito huo umetolewa leo jijini Dodoma na Kamishna Msaidizi wa Polisi Daniel Bendarugaho, alipokuwa akizungumza katika mkutano wa Polisi Wanawake uliofanyika kwa lengo la kutathmini utekelezaji wa majukumu yao na kuangalia namna ya kuimarisha uhusiano na jamii.

Bendarugaho amesema askari wa TPF NET wanapaswa kutambua nafasi yao katika jamii na kuhakikisha wanakuwa mfano wa kuigwa kupitia utendaji wao, mienendo na namna wanavyoshirikiana na wananchi.

Amesema uhusiano mzuri kati ya polisi na wananchi ni muhimu katika kurahisisha utekelezaji wa majukumu ya Jeshi la Polisi, hususan katika masuala ya ulinzi na usalama.


Kwa mujibu wa Bendarugaho, Polisi Wanawake wanapaswa kutumia shughuli mbalimbali za kijamii kama fursa ya kuwafikia wananchi, kuwasikiliza na kuelewa changamoto zinazowakabili katika maeneo yao.

Amesema hatua hiyo pia itasaidia kuongeza ushirikiano wa wananchi na Jeshi la Polisi katika kutoa taarifa na kushiriki katika jitihada za kuzuia uhalifu.

Kwa upande wake, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Mossi Ndozero amesema TPF NET imekuwa ikifanya kazi kwa kushirikiana na makundi mbalimbali ya kijamii katika kutekeleza shughuli zenye manufaa kwa wananchi.

Ndozero amesema miongoni mwa shughuli zinazofanywa na mtandao huo ni usafi katika shule, kuwatembelea wagonjwa hospitalini pamoja na kutoa misaada katika vituo vya watoto yatima.

Amesema shughuli hizo ni sehemu ya jitihada za Polisi Wanawake kuendelea kuwa karibu na jamii na kuonyesha kwa vitendo dhamira yao ya kushiriki katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.

Ndozero amesisitiza kuwa kuimarishwa kwa shughuli hizo kutasaidia kujenga mahusiano yenye tija kati ya Polisi Wanawake na jamii, jambo litakalochangia kwa kiasi kikubwa katika utekelezaji wa majukumu ya ulinzi na usalama.





 

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3