Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
SERIKALI KUENDELEA KUUNGA MKONO TAASISI ZINAZOWEZESHA MAENDELEO YA KILIMO

SERIKALI KUENDELEA KUUNGA MKONO TAASISI ZINAZOWEZESHA MAENDELEO YA KILIMO


 Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma

SERIKALI imesema itaendelea kuunga mkono taasisi zinazowezesha maendeleo ya sekta ya kilimo ili kuongeza uzalishaji, kuimarisha usalama wa chakula na kukuza uchumi wa taifa.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Hamad Chande, alipotembelea banda la Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma.

Mhe. Chande amesema sekta ya kilimo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa nchi na chanzo kikuu cha ajira kwa Watanzania wengi, hivyo Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi zinazowezesha upatikanaji wa huduma za kifedha na uwekezaji katika sekta hiyo.

Amepongeza TADB kwa kuendelea kutekeleza jukumu lake la kuchochea maendeleo ya kilimo kupitia utoaji wa huduma za kifedha zinazowawezesha wakulima, wafugaji na wadau wengine wa mnyororo wa thamani wa kilimo kuongeza uzalishaji na tija.

Amesema mchango wa benki hiyo unaendelea kuimarisha usalama wa chakula, kuongeza kipato cha wananchi na kuchangia ukuaji wa uchumi kupitia maendeleo ya sekta ya kilimo.

Akiwa katika banda la TADB, Naibu Waziri amepata maelezo kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na benki hiyo, ikiwemo mikopo kwa wakulima na wawekezaji wa sekta ya kilimo pamoja na programu zinazolenga kuwawezesha vijana, wanawake na wajasiriamali wa kilimo.

Maonesho ya Nanenane yameendelea kuwa jukwaa muhimu kwa taasisi za umma na binafsi kuonesha teknolojia, huduma na fursa mbalimbali zinazochochea maendeleo ya sekta ya kilimo, huku TADB ikiwa miongoni mwa taasisi zinazotoa elimu na huduma za kifedha kwa wadau wa sekta hiyo.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3