JKT YABADILI MTAZAMO WA VIJANA KUHUSU KILIMO, UFUGAJI NA UVUVI
Na Lilian Kasenene, Morogoro
Matukio DaimaApp
JESHI la Kujenga Taifa (JKT) limesema limejikita katika kubadilisha mtazamo wa vijana wanaoona kilimo ni kazi ya watu wa vijijini na wazee, badala yake kuwahamasisha kutumia fursa hiyo kujiajiri kupitia kilimo, ufugaji na uvuvi.
Hayo yalisemwa na mwakilishi wa mkuu wa Jeshi la kujenga Taifa JKT,Kanali Cleopatra Callistus Nazar wa JKT alitembelea vipando na mabanda ya jeshi hilo katika viwanja vya Maonyesho ya NaneNane vya JKT mjini Morogoro.
"Mbali na kuwafundisha masuala ya ulinzi na usalama wa nchi na raia wake, pia tumewekeza kuwajenga vijana kutumia fursa zilizopo katika kilimo, ufugaji na uvuvi ili waweze kujiajiri wenyewe," alisema.
Alisema JKT linawajengea vijana imani kwamba wanaweza kujiajiri kwa kutumia zana na teknolojia za kisasa katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi.
Aliongeza kuwa vijana wengi wanaopitia mafunzo ya JKT wana uwezo wa kujiajiri katika sekta mbalimbali nchini na kwamba wameondokana na mtazamo hasi kuwa ajira zinapatikana serikalini pekee.
Mmoja wa vijana waliopitia mafunzo ya JKT, Miriam Abdull, alisema mafunzo aliyoyapata yamebadili fikra zake kwamba kilimo, ufugaji na uvuvi ni kazi za wazee.
"Awali ukiniambia niwe mkulima au mfugaji nilikuwa naona ni ushamba, ni kazi za watu wa vijijini. Kwa elimu niliyoipata JKT, kwa sasa nipo mjini lakini nalima bustani ndogondogo," alisema Miriam.
Alisema kilimo walichojifunza kinazingatia matumizi ya zana za kisasa, ambapo kwa kutumia eneo dogo mtu anaweza kupata mazao mengi na yenye tija.
*Mwisho.*
