BODI YA BIMA YA AMANA: KILA MWEKAJI ANASTAHILI FIDIA HADI SH. MILIONI 7.5
Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media, Dodoma
BODI ya Bima ya Amana (DIB) imesema kiwango cha juu cha fidia kinacholipwa kwa kila mwekaji fedha ni Shilingi milioni 7.5 endapo benki au taasisi ya fedha yenye leseni ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) itafutiwa leseni na kushindwa kuendelea na shughuli zake.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa Bodi ya Bima ya Amana, Lwaga Mwambande, wakati akitoa elimu kwa wananchi waliotembelea banda la taasisi hiyo katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.
Mwambande amesema wananchi wanaoweka fedha katika benki zenye leseni ya Benki Kuu ya Tanzania wanakuwa wamenufaika moja kwa moja na kinga ya bima ya amana, bila kulazimika kulipa gharama yoyote, kwani michango ya mfuko huo hutolewa na benki na taasisi za fedha wanachama.
Amesema benki zote zinazopokea amana kutoka kwa wananchi huchangia asilimia 0.15 ya amana zao kila mwaka katika Mfuko wa Bima ya Amana, huku fedha hizo zikiwekezwa katika dhamana za Serikali na maeneo mengine salama ya uwekezaji ili kuhakikisha mfuko unakuwa na uwezo wa kulipa fidia pale inapohitajika.
Aidha, amefafanua kuwa mteja mwenye amana inayozidi Shilingi milioni 7.5 hapotezi fedha zake zote, kwani baada ya benki kufungwa huanza mchakato wa ufilisi ambapo mali za benki hukusanywa na kugawiwa wadai kwa mujibu wa sheria.
Amesema mbali na kulipa fidia kwa wateja wa benki zilizofungwa, Bodi ya Bima ya Amana pia ina jukumu la kusaidia benki zinazokabiliwa na changamoto za kifedha kabla hazijafikia hatua ya kufutiwa leseni, ikiwemo kutoa mtaji, dhamana au mikopo ili kuzinusuru.
Kwa upande wake, Meneja wa Fedha na Uhasibu wa Bodi ya Bima ya Amana, Romuli Mtui, amesema benki tisa zimewahi kuwekwa chini ya ufilisi nchini, zikiwemo Greenland Bank, Delphi Bank, FBM Bank, Mbinga Community Bank, Njombe Community Bank, Meru Community Bank, Kagera Farmers' Cooperative Bank, Efatha Community Bank na FDM Bank.
Mtui amesema Bodi imeendelea kulipa fidia kwa wateja wa benki zilizofungwa na kuwahimiza wale ambao bado hawajachukua malipo yao kufuatilia katika ofisi za Bodi ya Bima ya Amana zilizopo ndani ya Benki Kuu ya Tanzania, Dar es Salaam na Dodoma au kupitia njia rasmi za mawasiliano za taasisi hiyo.
Aidha, amewataka wateja wenye amana zinazozidi kiwango cha fidia kuendelea kufuatilia mchakato wa ufilisi ili waweze kulipwa fedha zao kulingana na mali zitakazopatikana na taratibu za kisheria.

