MZOZO WA UKRAINE: URUSI YAIONYA UINGEREZA - KUNANI?
Urusi imeishutumu Uingereza kwa "kuchochea mzozo wa Ukraine" kufuatia uthibitisho kwamba ndege zisizo na rubani zilizotengenezwa Uingereza zilitumika kushambulizi maeneo yaliyolengwa nchini Urusi.
"Kwa kufanya hivyo, Uingereza inashiriki kama msaidizi na mhusika mwenza katika uhalifu wa umwagaji damu na mashambulizi ya kigaidi," ilisema taarifa kutoka Ubalozi wa Urusi nchini Uingereza.
"London bila shaka italazimika kuwajibikia hatua yake," ilisema taarifa hiyo, huku ikiongeza kuwa kadiri inavyozidi kujihusisha na mgogoro huo, "ndivyo gharama itakayolipa itakavyokuwa kubwa zaidi."
Msemaji wa Wizara ya Ulinzi (MoD) amembia BBC kuwa Uingereza inasimama "bega kwa bega" na Ukraine.
"Urusi haipaswi kuwa na shaka yoyote kuhusu azimio la Serikali hii la kupinga uchokozi wa wake, iwe ni nchini Ukraine au dhidi ya Uingereza na washirika wetu," alisema msemaji huyo katika taarifa.
Uingereza iliongeza kuwa "imejitolea kutoa vifaa ambavyo Ukraine inahitaji ili kujilinda dhidi ya uvamizi haramu wa [Rais wa Urusi Vladimir] Putin".
Ndege hizo zisizo na rubani zilizotengenezwa na kampuni mbili tofauti za Uingereza zimetumika kushambulia kwa mafanikio vituo vya kijeshi na viwandandani ya Urusi, ikiwemo mitambo ya kusafisha mafuta na maghala ya kampuni ya mauzo ya mtandaoni ya Wildberries.
Ukraine imekuwa ikilenga mara kwa mara kampuni hiyo —ambayo inajulikana kama toleo la Urusi la Amazon—na kusema kuwa vituo saba kati ya 10 vikubwa zaidi vya usafirishaji na uhifadhi bidhaa vya Wildberries "vimesambaratishwa".