Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
 UPANUZI UWANJA WA NDEGE SINGIDA WAANZA KWA FIDIA

UPANUZI UWANJA WA NDEGE SINGIDA WAANZA KWA FIDIA


‎Elisante John, Singida,

‎‎Hatua ya Serikali kupanua Uwanja wa Ndege wa Singida imeibua ombi kutoka kwa wananchi, kuondolewa kwenye maeneo yao, wakiomba thamani ya ardhi inayotumika katika fidia, ipandishwe kutoka Sh. 8,000 hadi Sh.10,000, kwa mita ya mraba.

‎‎Mthamini wa Ardhi Mkoa wa Singida, Zablon Mwalyasi, amesema upanuzi huo unahusisha kuongeza ekari 316.6 kutoka maeneo ya wananchi yaliyo pembezoni mwa uwanja. Amesema lengo ni kuboresha huduma za usafiri wa anga, kwa kuwa uwanja uliopo hautoshelezi mahitaji ya sasa.


‎Mwalyasi amesema kila mwananchi atakayepitiwa na zoezi hilo atalipwa fidia kwa kuzingatia thamani halisi ya ardhi na mali zilizopo. Amesema mali hizo ni pamoja na majengo, miti na maendeleo mengine yanayotambuliwa kisheria.

‎‎Ameongeza kuwa wananchi watastahili pia posho mbalimbali, ikiwamo ya usumbufu, makazi, upangaji na gharama za kuhamisha mali. Amewataka wananchi kuwa wazi wakati wa uthamini na kuwaruhusu wataalamu kukagua mali zote ili kuhakikisha thamani halisi inapatikana.




‎Baadhi ya wananchi, akiwamo Charles Rwegoshora, Shabani Nyuda, Karani Kisuke, Hassan Irunde na Diwani wa Kata ya Mandewa, Yusufu Makera, wameomba thamani hiyo ipandishwe kutoka Sh. 8,000 hadi Sh10,000, kwa mita ya mraba. Mwalyasi amesema atalifikisha ombi hilo kwa mamlaka husika kwa ajili ya uamuzi.

‎‎Kwa upande wake, mwakilishi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Singida, Bornege Tatwebwa, amesema upanuzi wa uwanja huo utaongeza fursa za usafiri wa anga na kuchochea maendeleo ya kiuchumi. Pia amewapongeza wananchi kwa ushirikiano wanaouonesha katika kuunga mkono zoezi hilo.





Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3