VIJANA NA MAMA LISHE WANUFAIKA MKOPO IRAMBA, SINGIDA
Na Elisante John, Matukiodaima Singida,
Vijana wa Kijiji cha Makunda, Wilaya ya Iramba, wamepatiwa Sh263 milioni kwa ajili ya kuboresha kiwanda cha kukamua mafuta ya alizeti, hatua inayolenga kuongeza uzalishaji, ajira na thamani ya zao hilo katika eneo analotoka na kuzaliwa Waziri Mkuu wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba.
Fedha hizo ni sehemu ya Sh.363/- milioni zilizotolewa na Serikali kwa vijana na wanawake mkoani Singida, kupitia mpango wa mikopo unaotokana na Sh.200/- bilioni zilizotengwa kwa ajili ya kuwawezesha vijana nchini, kujikwamua kiuchumi.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya mikopo hiyo, uliofanyika Kijiji cha Makunda, wilaya ya Iramba, Waziri wa Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, amesema Sh.263/- milioni zilizotolewa kwa vijana wa Kijiji hicho, zitatumika kuboresha kiwanda hicho, ikiwemo kupatiwa mashine kubwa na ndogo za kuchakata alizeti, gari la tani saba na mtaji wa kununua zao hilo
kutoka kwa wakulima.
Nanauka amesema gari hilo lina thamani ya zaidi ya Sh.97.6/- milioni na litatumika kusafirisha alizeti pamoja na kusambaza mafuta kwa haraka sokoni. Aidha, sehemu ya fedha hizo, Sh.100/- milioni zitatumika kama mtaji wa kununua alizeti shambani, hatua inayolenga kuhakikisha kiwanda kinapata malighafi ya kutosha kwa uzalishaji.
Waziri huyo amesema Serikali inalenga kuongeza thamani ya mazao ya ndani na kupunguza utegemezi wa mafuta ya kula yanayoagizwa kutoka nje ya nchi. Ameongeza kuwa vijana wanapaswa kutumia fursa hizo kuanzisha na kukuza biashara pamoja na viwanda vitakavyoongeza ajira na kuchangia uchumi.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Vijana, Dkt. Reginald Malima, amesema baada ya kutembelea vikundi mbalimbali vya vijana Iramba, na kujionea shughuli zinazofanyika, amesema juhudi hizo zinaweza kuwa mfano wa kuigwa na wilaya nyingine nchini, hiku pia akiitaka Serikali ya Wilaya ya Iramba kuwawezesha vijana kupata maeneo ya ardhi kwa ajili ya kuendeleza na kupanua shughuli zao, ikiwemo viwanda, ili waweze kutumia kikamilifu fursa za kiuchumi zilizopo katika wilaya hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda, amesema wilaya hiyo ina zaidi ya vikundi 246 vya vijana vilivyosajiliwa vinavyojishughulisha na ufundi, biashara na shughuli nyingine za kiuchumi, huku zao la alizeti likiwa miongoni mwa shughuli zinazotoa fursa nyingi kwa vijana. Katika hafla hiyo, Serikali pia ilikabidhi Sh.100/- milioni kwa wanawake wanaojishughulisha na biashara ya mama lishe katika Manispaa ya Singida, huku wanufaika akiwemo Janifa David na Orgenes Yindi, wakisema mikopo hiyo itasaidia kuongeza uzalishaji na kukuza shughuli zao.
Meneja Biashara wa CRDB Kanda ya Kati, Andrew Mheziwa, amesema benki hiyo imepewa jukumu la kusaidia mchakato wa kuwawezesha vijana, ikiwemo kuwachambua wanaokidhi vigezo na kuwapatia mafunzo ya biashara, ili kuweza kumudu shughuli zao za biashara.
MWISHO





