Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
MBEGU BORA ZA ASA ZAONGEZA MATUMAINI YA MAVUNO KWA WAKULIMA.

MBEGU BORA ZA ASA ZAONGEZA MATUMAINI YA MAVUNO KWA WAKULIMA.

 

NA CHAUSIKU SAID 

MATUKIO DAIMA MWANZA.

WAKALA wa Mbegu za Kilimo (ASA) wameeleza kuwa matumizi ya mbegu bora zilizothibitishwa yameendelea kuongeza tija kwa wakulima nchini, huku wakitoa wito kwa wakulima kujiandaa mapema kwa msimu wa kilimo wa 2026/2027 ili kuongeza uzalishaji wa mazao.

Akizungumza katika Maonesho ya Kilimo na Sherehe za Wakulima (Nanenane) yanayoendelea katika viwanja vya Nyamhongolo jijini Mwanza, Afisa Masoko wa ASA, Wakirya John alisema taasisi hiyo imeshiriki maonesho hayo kwa lengo la kutoa elimu ya matumizi sahihi ya mbegu bora pamoja na kusogeza huduma ya mbegu karibu na wakulima.

Wakirya ameeleza kuwa Kanda ya Ziwa imeendelea kuwa miongoni mwa maeneo yenye matumizi makubwa ya mbegu zinazozalishwa na ASA, hususani mbegu za mpunga SARO 5 pamoja na mbegu za mahindi SITUKA M1 na T105 ambazo zimeonyesha kufanya vizuri katika mazingira ya ukanda huo.

"Katika kila msimu wa Nanenane tumekuwa tukishuhudia mwitikio mkubwa wa wakulima Safari hii pia wakulima wengi wamefika kwenye banda letu kupata elimu na mbegu bora zinazozalishwa na ASA, taasisi ya Serikali," Alisema Wakirya.

Alieleza kuwa ASA haitoi mbegu pekee, bali huwapatia wakulima elimu ya kina kuhusu hatua zote za uzalishaji kuanzia uchaguzi wa mbegu, maandalizi sahihi ya shamba, matumizi ya mbolea hadi usimamizi wa zao, ili kuhakikisha wanapata mavuno yenye tija.

Kwa mujibu wa Wakirya, mkulima anayelima mbegu ya mahindi T105 na kuifuata kanuni za kilimo bora anaweza kuvuna kati ya magunia 28 hadi 30 kwa ekari, huku mbegu ya mpunga SARO 5 ikiwawezesha baadhi ya wakulima kuvuna kati ya magunia 30 hadi 50 kutokana na ushuhuda wa wakulima waliotembelea banda la ASA.

Alisema ASA inaendelea kushirikiana na kampuni binafsi kuhakikisha mbegu bora zinapatikana kwa wakati, huku akibainisha kuwa mbegu zote zinazosambazwa na wakala huo zimethibitishwa na Taasisi ya Udhibiti wa Ubora wa Mbegu Tanzania - TOSCI.

"Tunawasihi wakulima kujiandaa mapema kabla ya msimu kuanza waandae mashamba yao vizuri kwa kufanya maandalizi yote muhimu, ikiwemo kulima na kufanya halo kwa wakati. Shamba lisipoandaliwa vizuri hata mbegu bora inaweza isitoe matokeo yaliyokusudiwa," Alisema wakirya.

Aidha, alisema ASA tayari imesambaza mbegu zake zilizothibitishwa katika kanda mbalimbali nchini ili kuhakikisha wakulima wanazipata mapema na kuanza msimu wa kilimo wa 2026/2027 kwa wakati.

Naye mkulima Samson Moleli, ambaye amesema amekuwa akitumia mbegu za ASA kwa zaidi ya miaka 20, alieleza kuwa matumizi ya mbegu hizo yamebadili kwa kiasi kikubwa uzalishaji wake.

Alisema kabla ya kutumia mbegu za ASA alikuwa akitegemea mbegu za kienyeji zilizokuwa zikitoa mavuno duni na kushambuliwa kirahisi na magonjwa na wadudu.

"Baada ya kuanza kutumia mbegu za SITUKA za ASA, mavuno yameongezeka sana Kwa ekari moja sasa ninapata hadi magunia 15, tofauti na zamani nilipokuwa napata magunia 5 hadi 8 kwa kutumia mbegu za kienyeji, hizi ni mbegu zilizofanyiwa utafiti na zina uwezo mkubwa wa kustahimili magonjwa na wadudu,"Alisema Moleli.


Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3