Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
 CHOMO AWATAKA WATENDAJI, MADIWANI ILEJE KUHAMASISHA VIJANA KUCHAPA KAZI.

CHOMO AWATAKA WATENDAJI, MADIWANI ILEJE KUHAMASISHA VIJANA KUCHAPA KAZI.


Na Moses Ng’wat, Ileje.

MWENYEKITI wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje, Osiwelo Chomo, amewataka watendaji wa kata, madiwani na wataalamu wa halmashauri hiyo kutumia uelewa na taaluma zao kuhamasisha jamii, hususan vijana, kujenga utamaduni wa kufanya kazi na kujikita katika shughuli za uzalishaji.

Chomo alitoa kauli hiyo Agosti 4, 2026 wakati akifunga kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje, kilicholenga kupitia na kujadili taarifa za robo ya nne ya mwaka wa fedha 2025/26.

Alisema vijana wanapaswa kuhamasishwa kutumia muda wao katika shughuli zenye tija badala ya kujihusisha na mambo yasiyokuwa na mchango katika maendeleo yao binafsi na jamii kwa ujumla.

“Tunapaswa kuwahamasisha vijana kufanya kazi kwa bidii, kwa sababu kupitia uzalishaji ndipo wataweza kujiletea maendeleo yao na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii,” alisema Chomo.

Katika hatua nyingine, Chomo aliviasa vyombo vya ulinzi na usalama wilayani humo kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya haki, sheria na taratibu ili kuepusha malalamiko yasiyo ya lazima kutoka kwa wananchi.

Alisema katika operesheni na misako inayofanyika kwenye maeneo mbalimbali, ni muhimu watendaji wa vitongoji, vijiji na kata kushirikishwa ili kuimarisha mawasiliano, uwazi na ushirikiano kati ya vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wananchi.

Awali, Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ileje, Hassan Lyamba, alisema chama hicho kimeridhishwa na utendaji wa Serikali katika ngazi mbalimbali, hususan utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia fedha zinazotolewa na Serikali.

Lyamba aliwapongeza wataalamu wa halmashauri kwa usimamizi mzuri wa fedha na juhudi za ukusanyaji wa mapato ya ndani, ambapo alisema halmashauri hiyo imefikia asilimia 107 ya lengo la makusanyo.

Hata hivyo, aliwataka wataalamu hao kuongeza ubunifu na kasi katika ukusanyaji wa mapato ili kuendelea kuimarisha uwezo wa halmashauri katika kutoa huduma na kutekeleza miradi kwa wananchi.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Ileje, Abdala Mayomba, akitoa salamu za Serikali kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo, aliwataka madiwani na watendaji wa kata kuhakikisha wanasikiliza na kutatua kero za wananchi kwa wakati.

Mayomba pia alisisitiza umuhimu wa kulinda amani, akieleza kuwa utulivu ni msingi muhimu wa maendeleo na kila mwananchi ana wajibu wa kushiriki katika kuudumisha.

Mwisho.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3