MASHAMBULIZI YA WAHOUTHI YARIPOTIWA KUUA WANAJESHI 30 WA SERIKALI YA YEMEN
Inaripotiwa kuwa takriban askari 30 wa serikali ya Yemen wameuawa katika mashambulizi yaliyofanywa na waasi wa Houthi dhidi ya kambi za kijeshi katikati mwa Yemen.
Wizara ya Ulinzi ilisema kuwa makombora ya masafa marefu na ndege zisizo na rubani (drones) zililenga kambi kadhaa katika mikoa ya Marib na Hadramawt, na kusababisha vifo na majeraha kwa idadi ya askari wa Yemen.
Wizara hiyo haikutaja idadi kamili ya waathiriwa.
Wizara hiyo ililaani mashambulizi hayo na kuyaelezea kuwa ya "hila na usaliti" na kuahidi "kujibu uchokozi huu wakati na mahali mwafaka".
Kundi la Houthi, ambalo linadhibiti sehemu kubwa ya kaskazini-magharibi mwa Yemen na kuungwa mkono na Iran, lilisema kuwa lililenga "vikosi vikubwa vya kijeshi vya Saudi Arabia" vilivyokuwa vikijiandaa kwa operesheni ya kijeshi.
Muungano unaoongozwa na Saudi Arabia umekuwa ukiunga mkono serikali wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Katika shambulio jingine tofauti, msemaji wa muungano huo alisema kuwa raia 11 walijeruhiwa katika eneo la mpakani la Najran nchini Saudi Arabia, katika tukio walilolielezea kuwa shambulio la Houthi.
Katika taarifa yao iliyochapishwa kwenye mtandao wa X, walisema kuwa miongoni mwa waliojeruhiwa kulikuwa na raia saba wa Saudi Arabia, akiwemo mwanamke na mtoto wa miaka minne ambao wote walipata majeraha ya kuungua ngozi kwa kiwango cha pili.
Raia wengine wanne walikuwa kutoka Yemen, Pakistan na Misri.
Mashambulizi ya Houthi katikati mwa Yemen yalifanyika saa 10:40 kwa saa za eneo hilo (saa 07:40 GMT) siku ya Alhamisi, kulingana na Wizara ya Ulinzi ya Yemen.