Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
 MADIWANI CHUNYA WAONYWA KUTIMIZA WAJIBU WAO.

MADIWANI CHUNYA WAONYWA KUTIMIZA WAJIBU WAO.


Na Samwel Mpogole - Mbeya.

Mkuu wa Wilaya ya Chunya Mhe.Mbaraka Alhaji Batenga amewataka madiwani kutambua wajibu wao wa kuwawakilisha wananchi kwa kuhakikisha wanahudhuria vikao vya Baraza la Madiwani na kushiriki kikamilifu katika kufanya maamuzi ya maendeleo.

Hayo yanajiri baada ya zaidi ya madiwani 10 kutoshiriki kikao maalumu cha Baraza la Madiwani kilichokutana kujadili na kupitisha hesabu za mwisho za Halmashauri kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

Mbali na suala la mahudhurio, Mkuu huyo wa Wilaya amewataka madiwani kuhakikisha wanabaini maeneo yenye changamoto ya maji na kuweka mipango maalumu ya uchimbaji wa mabwawa, akisisitiza kuwa mitambo ya uchimbaji ipo na hivyo kinachohitajika ni kuwasilisha maombi ya maeneo yenye uhitaji.

Pia, amewataka madiwani kushirikiana na wananchi na watendaji katika kujiandaa kupokea wahitimu wa darasa la saba na darasa la sita wanaotarajiwa kujiunga na elimu ya sekondari, ambapo Halmashauri ina uhitaji wa vyumba vya madarasa 141 na matundu ya vyoo 577, huku zaidi ya shilingi bilioni tatu zikihitajika kukidhi mahitaji hayo.

Kadhalika, madiwani wametakiwa kusimamia upangaji bora wa huduma za kibiashara, ikiwemo kutenga maeneo rasmi kwa ajili ya shughuli za wachomeleaji na ujenzi wa parking, ili kuhakikisha mji wa Chunya unakuwa salama na wenye mpangilio.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Bwana Kelvin Shinshi, amewaagiza madiwani kuhakikisha wanasimamia vyema wananchi wanaowawakilisha na kufuatilia utekelezaji wa mipango ya maendeleo katika maeneo yao.

Amesema Halmashauri tayari imeanza kuchukua hatua za kutekeleza mipango ya kukabiliana na changamoto ya maji katika maeneo mbalimbali, huku akisisitiza kuwa kila diwani ana wajibu wa kuhakikisha mahitaji ya wananchi yanafikishwa na kufanyiwa kazi.

Kuhusu mahudhurio ya vikao, Mwenyekiti huyo amesema uvunjifu wa nidhamu unaosababishwa na kutohudhuria vikao hautaendelea kuvumiliwa, na kwamba hatua za kinidhamu zitaanza kuchukuliwa dhidi ya madiwani watakaokiuka kanuni na taratibu za mahudhurio.

Kwa upande wake, Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Chunya, Francis Michael, amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha kunakuwa na usimamizi madhubuti na wa ufanisi wa mapato ya Halmashauri, ili fedha zinazokusanywa zitumike kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa.

Amesema usimamizi wa mapato kwa uadilifu utasaidia kuzuia upotevu wa fedha na kuhakikisha rasilimali zinazokusanywa zinatumika kutekeleza miradi ya maendeleo na kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3