POLISI YAWATAKA WANANCHI KUWAJUA JIRANI ZAO
Na Lilian Kasenene, Morogoro
maipacarusha20@gmail.com
JESHI la Polisi nchini limewataka wananchi kuwajua majirani zao na wageni wanaoingia katika maeneo yao ili kulinda amani na kukomesha uhalifu.
Kamishna wa Polisi Jamii Tanzania, CP Alex Mukama, alisema hayo katika Tamasha la Nne la Utamaduni wa Tanzania linaloendelea mkoani Morogoro.
Alisema ni muhimu kila mwananchi kumtambua jirani yake na kufahamu wageni wanaoingia katika eneo lake, pamoja na kujua iwapo wapo nchini kihalali.
“Huku kuna Polisi Jamii, Uhamiaji wana kaulimbiu ya ‘Mjue Jirani’ na sisi ni nyumba moja. Lengo ni kuhakikisha kila Mtanzania anakuwa mlinzi wa amani popote alipo,” alisema CP Mukama.
Alisema wakati Jeshi hilo likiadhimisha miaka 20 tangu kuanzishwa kwa Polisi Jamii, limeendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kutunza amani, kupinga vitendo vya uhalifu na kufanya shughuli za kuinua uchumi.
“Hatuwakatai wageni, lakini ni lazima tujue kama wageni hao wako nchini kwa kufuata sheria na taratibu na kama shughuli zao zinatambulika,” alisema CP Mukama.
CP Mukama alilitaka Jeshi la Polisi kuendelea kutoa elimu kwa wananchi na kushirikiana na Polisi Jamii katika kukomesha uhalifu kwenye maeneo yao na taifa kwa ujumla.
Aliongeza kuwa Jeshi hilo pia linaendelea kutoa elimu kuhusu madhara ya biashara na matumizi ya dawa za kulevya kwa lengo la kulinda jamii, hasa vijana.
.jpeg)

.jpeg)

