Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
DODOMA YAZIDI KUFUNGUA MILANGO YA ELIMU KWA WANANCHI

DODOMA YAZIDI KUFUNGUA MILANGO YA ELIMU KWA WANANCHI

 


Na Hamida Ramadhani, Matukio Daima Media Dodoma


WANANCHI waliokosa nafasi ya kupata au kukamilisha elimu kupitia mfumo rasmi wameendelea kupata fursa ya kujifunza kupitia programu za Elimu ya Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi, zinazolenga kuwaongezea maarifa, ujuzi na uwezo wa kujitegemea.


Hayo yameelezwa Agosti 21, 2026, katika kilele cha Juma la Elimu ya Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi lililofanyika Viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma kuanzia Agosti 17 hadi 21, likihudhuriwa na Afisa Elimu Mkoa wa Dodoma, Kiduma Mageni, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa, Rosemary Senyamule.


Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mageni amesema Mkoa unaendelea kuimarisha programu hizo ili kuwafikia wananchi wengi zaidi, akibainisha kuwa Dodoma ina shule 976 za msingi na 308 za sekondari ambazo miundombinu yake pia hutumika kutoa elimu kwa wanafunzi wa programu za Elimu Nje ya Mfumo Rasmi.



Mageni amesema Mkoa pia una vyuo vitatu vya ualimu, vyuo viwili vya Ufundi Stadi (FDC) na vituo sita vya VETA, huku mwaka 2026 ukipokea zaidi ya Shilingi bilioni 22.5 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya BOOST, SEQUIP, SWASH na GPE-TSP.


Amesema Serikali inaendesha programu za MEMKWA, MESKWA, MUKEJA, IPOSA na Elimu Masafa, ambazo zimekuwa zikiwapatia wananchi stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu pamoja na ujuzi katika kilimo, ufugaji, ushonaji, ujasiriamali na utunzaji wa hesabu za biashara.


Ameongeza kuwa kupitia mpango wa SEQUIP-AEP, wanafunzi 537, wakiwemo wavulana 186 na wasichana 351, wamepata nafasi ya kurejea shuleni na kukamilisha elimu ya sekondari baada ya kukosa fursa hiyo katika mfumo rasmi, huku wakisoma bila kulipa ada wala gharama nyingine za masomo.



Kwa upande wake, Mratibu wa Elimu ya Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi, Borase Chibura, amesema maadhimisho hayo yanalenga kuongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa elimu hiyo na kuhamasisha wananchi kutumia programu zinazosaidia kukabiliana na changamoto za ujinga, umaskini na maradhi.


Chibura amesema Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuwapa fursa wanafunzi waliokatiza masomo kurejea shuleni kupitia SEQUIP-AEP, huku akisisitiza kuwa wanafunzi hao hawalipi ada wala gharama nyingine kwa kuwa elimu yao inagharamiwa na Serikali.


“Kwa sasa, Mkoa wa Dodoma una madarasa maalumu ya Elimu Mbadala kupitia mpango wa SEQUIP-AEP yenye jumla ya wanafunzi 537, wakiwemo wavulana 186 na wasichana 351,” amesema Chibura.



Aidha, wadau mbalimbali wakiwemo Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima, VETA, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, UNICEF na DVV International wametajwa kuwa na mchango mkubwa katika kuziba pengo la elimu, huku Mkoa ukiwataka wananchi na vijana kutumia fursa hizo kuongeza ujuzi na maarifa, na kuwahimiza wadau kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuimarisha Elimu ya Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3