MCHUNGAJI JONAM MSANGAWALE AWATAKA WANANDOA KUTHIBITISHA UPENDO KWA VITENDO
Furaha na shangwe zimetawala jijini Mbeya wakati Mzee Mwangosi na Christina wakifunga ndoa na kuanza rasmi safari mpya ya maisha, katika hafla iliyohudhuriwa na ndugu, jamaa, marafiki pamoja na waumini waliokwenda kushuhudia tukio hilo la kihistoria.
Katika ibada hiyo ya ndoa, Mchungaji Jonam Msangawale wa Kanisa la Moravian, aliyewafungisha wanandoa hao, alitumia nafasi hiyo kutoa nasaha mbalimbali kuhusu maisha ya ndoa, akisisitiza kuwa upendo wa kweli hauishii kwenye kutamka maneno ya “nakupenda”, bali unatakiwa kuonekana kupitia matendo ya kila siku.
Msangawale alisema wanandoa wanapaswa kujifunza kuelewana na kuthibitishiana upendo kwa vitendo, ikiwemo kuhakikisha usalama, furaha na ustawi wa mwenza wao. Alisema mtu anayempenda mwenza wake anapaswa kumfikiria na kujali mahitaji yake kabla ya kuangalia mambo mengine.
“Ikiwa unajua namna gani unavyompenda mwenzako utaudhihirisha kwa matendo huo Upendo pia utahakikisha usalama wake,utahakikisha furaha yake,utahakikisha kila wakati unamfikiria yeye kabla ya kufikiria mambo mengine”
Aidha, aliwataka wanandoa kuwa na utamaduni wa kuwasiliana katika mambo madogo ya kila siku, akitoa mfano wa mmoja wao anapotoka nyumbani kwenda sokoni au sehemu nyingine Alisema ni muhimu kumjulisha mwenza wake ili kujenga heshima, uaminifu na ushirikiano ndani ya familia.
“Kwa wanandoa wote mliopo mama au baba,Mwanamke unapoondoka kwenda sokoni na mume wako yupo hapo nyumbani usiondoke tu bila kumjulisha maana anaweza kuanza kutafuta mama Fulani ameenda wapi hiyo inakuwa sio vizuri ni vizuri kutoa taarifa kwa kufahamishana kwamba kuna mahali unaenda ila hata ikitokea changamoto iwe rahisi kuweza kusaidia.”
Pia Msangawale alisisitiza umuhimu wa wanandoa kuulizana mahitaji yao badala ya kufanya maamuzi kila mmoja peke yake Alisema kuuliza mwenza anataka kula nini ni sehemu ya kuonyesha upendo na kumfanya ajisikie anathaminiwa ndani ya ndoa.
Aidha alizungumzia suala la zawadi na mavazi, akiwataka wanandoa kuelewa mahitaji na mapendeleo ya wenzao kabla ya kununua vitu kwa ajili yao Alisema zawadi inaweza kuwa ishara nzuri ya upendo, lakini ni muhimu pia kuzingatia kile ambacho mwenza anakihitaji na kukipenda.
Pia alisisitiza kuwa somo la ndoa si kwa wale wanaofunga ndoa pekee, bali ni kwa kila mmoja katika jamii, wakiwemo vijana, wazee, wajane na wale ambao bado hawajaoa au kuolewa. Alisema kila mmoja anaweza kujifunza namna ya kujenga mahusiano yenye upendo, heshima, mawasiliano na kusaidiana.
“Kila mtu ni mwanandoa mtarajiwa kwahiyo hata nyinyi mliopo hapa haya mafundisho yanawahusu usiseme kwamba mimi sipo kwenye ndoa kwahiyo haya hayanihusu hivyo kila mmoja anatakiwa ajifunze ndoa sawa na mwingine”
Hatahivyo mara baada ya ibada hiyo Msangawale aliwatakia Baraka Mzee Mwangosi na Christina kuanza maisha yao ya ndoa wakiwa na msingi wa upendo unaoonekana kwa vitendo, kuheshimiana na kusikilizana. Akisisitiza kuwa ndoa yenye furaha hujengwa na mambo madogo yanayofanywa kwa nia njema kila siku.














