Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
WAZAZI WATAKIWA KUWEKEZA KIMAADILI KWA WATOTO

WAZAZI WATAKIWA KUWEKEZA KIMAADILI KWA WATOTO

 



WAZAZI na walezi nchini wametakiwa kuacha kutegemea elimu ya darasani pekee kama muarobaini wa kuleta mabadiliko ya kimaadili kwa watoto wao na  badala yake, wameshauriwa kuwekeza nguvu katika kuwajenga watoto kisaikolojia na kitabia ili waje kuwa mfano mwema na kioo katika jamii inayowazunguka.


Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Taasisi ya Kutetea Haki na Maendeleo ya Vijana ya ‘Kijana Kwanza’, Abedi Mujibu, alipokuwa mgeni rasmi katika mahafali ya Shule ya Msingi Uhuru iliyopo Manispaa Moshi mkoani Kilimanjaro ambapo Alisema kuwa malezi bora yanaenda sambamba na upendo  na ushirikiano kutoka kwa wazazi.


"Hatuwezi kuwa na jamii bora ya kesho kama tutaiachia shule pekee jukumu la kulea, Elimu ya darasani inatoa maarifa ya kitaaluma, lakini maadili yanatengenezwa nyumbani, Wazazi lazima mtoe upendo, ushirikiano, na muweke mazingira rafiki yatakayomfanya mtoto afunguke na kujengwa kiroho na kiakili," alisema Mujibu.



Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa, mmomonyoko wa maadili unaoshuhudiwa sasa unachangiwa na baadhi ya wazazi kususia majukumu yao ya msingi. Alisisitiza kuwa kila mtu kwenye jamii ana wajibu wa kumlinda mtoto dhidi ya ukatili wa kijinsia na wa kimwili ambao umekuwa ukiongezeka siku hadi siku.


"Kila mmoja wetu anapaswa kuwa mlinzi wa mtoto wa mwenzake. Ni lazima tuhakikishe tunawalinda na matukio ya kikatili ambayo yamekuwa yakifanyiwa watoto hawa katika jamii zetu. Ukiona mtoto anafanyiwa ukatili, usinyamaze kwa kudhani si wako; mtoto wa mwenzio ni wako pia," alisisitiza Mujibu.


Kwa upande wake, Afisa Elimu Kata ya Mawenzi, Christopher Heri, aliunga mkono hoja hiyo na kueleza kuwa usalama wa mtoto unaanza pale mzazi anapojua mwenendo wake wa kila siku, iwe akiwa shuleni au nyumbani. Alisema ulinzi wa mtoto si wa mwalimu pekee, bali ni ushirikiano wa pande zote mbili.

"Ni jukumu la kila mzazi kuhakikisha watoto wanaendelea kujengwa katika misingi salama na kuwa salama wakati wote. Serikali inafanya kazi yake, walimu wanafanya yao, lakini kama mzazi hafuatilii mtoto wake anashinda wapi na anafanya nini baada ya masomo, juhudi hizi zote zitagonga mwamba," alisema Heri.



Naye Mkuu wa Shule ya Msingi Uhuru akizungumzia maendeleo ya shule hiyo, aliishukuru serikali kwa kuendelea kuleta fedha za  kuboresha miundombinu ya shule na kusema kwa milioni mia mbili thelathini na moja kwa ajili ya  mradi wa ujenzi wa Madarasa mapya  manne na ukarabati wa madarasa mengine saba.


Amesema kuwa kutokana na ukarabati wa madara hayo umeondoa msongamano wa wanafunzi darasani na mindominu Imekuwa mizuri na yakuvutia mazingira ya shule 


"Hali ilikuwa mbaya kiasi fulani kwa sababu shule hii ilikuwa ni ya zamani na baadhi ya majengo yalikuwa ni ya zamani sana na wanafunzi pia ni wengi ,namba ilikuwa ni kubwa na msongamano ulikuwa ni mkubwa kwa hiyo ukiangalia pia kwenye ukarabati wa madarasa haya yamesaidia kuboresha miundombinu ambayo ilikuwepo "alisema Kisima.



Hata hivyo, pamoja na mafanikio hayo ya miundombinu, shule hiyo bado inakabiliwa na changamoto kubwa ya kiusalama. Akisoma risala ya wahitimu mbele ya mgeni rasmi, mwanafunzi Nachma Nuru alibainisha kuwa ukosefu wa uzio unahatarisha usalama wao.


"Tunamshukuru Mungu kuwa wanafunzi tumeweza kufanikiwa katika nyanja mbalimbali za kimasomo na michezo. Pamoja na mafanikio haya makubwa, bado tunakabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa uzio wa kuzunguka shule yetu, hali inayosababisha muingiliano usio salama na kuhatarisha usalama wa wanafunzi na mali za shule," alisema Nachma katika risala yake.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3