Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
ZAIDI YA RAIA WA KIGENI ELFU 50 WAKIMBIA VURUGU AFRIKA KUSINI

ZAIDI YA RAIA WA KIGENI ELFU 50 WAKIMBIA VURUGU AFRIKA KUSINI

 

Zaidi ya raia wa kigeni 53,000 wameondoka au kurejeshwa katika nchi zao tangu Afrika Kusini ilipoanzisha operesheni maalumu ya kusimamia uhamiaji wiki tano zilizopita, mamlaka za nchi hiyo zimesema.

Maafisa wa serikali wanasema wengi wa waliorejeshwa wanatoka Malawi, Zimbabwe na Msumbiji. Wengine bado wanazuiliwa katika vituo vya muda wakisubiri kukamilika kwa taratibu za kurejeshwa makwao.

Operesheni hiyo ni miongoni mwa hatua kubwa zaidi kuwahi kuchukuliwa dhidi ya wahamiaji wasio na vibali nchini Afrika Kusini katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni. Inafuatia wiki kadhaa za maandamano ya kupinga uhamiaji yaliyogubikwa na vurugu, vitisho na matukio ya uporaji.

Waandamanaji wanaitaka serikali kuimarisha ulinzi wa mipaka na kuwafukuza wahamiaji wasio na vibali, wakidai kuwa wamechangia kuongezeka kwa ukosefu wa ajira, uhalifu na kuzorota kwa huduma za umma.

Hata hivyo, Umoja wa Mataifa umeonya dhidi ya kuwalaumu wahamiaji kwa changamoto za kijamii na kiuchumi zinazoikabili Afrika Kusini.

Makundi yanayopinga uhamiaji yameahidi kuendelea na maandamano ya kila wiki hadi serikali itakapotekeleza madai yao. Hali hiyo imeibua hofu ya kuzuka kwa vurugu zaidi.

Waandamanaji walikuwa wametoa kile walichokiita tarehe ya mwisho isiyo rasmi ya Juni 30 kwa wahamiaji wasio na vibali kuondoka nchini, hatua iliyowafanya maelfu ya wageni kuondoka kwa hofu ya kushambuliwa au kutishiwa.

Katika majuma ya hivi karibuni, nchi kadhaa zikiwemo Ghana, Nigeria, Uganda na Kenya zimewarejesha raia wao waliokuwa nchini Afrika Kusini.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3