WIZARA YA ELIMU YAWEKA MIKAKATI MIPYA KUFIKIA DIRA YA TAIFA 2050
Dodoma.
Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma
WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeanza kuweka mikakati mipya ya kuboresha sekta ya elimu ili iendane na mahitaji ya taifa na mabadiliko ya dunia, huku ikisisitiza umuhimu wa mapitio ya programu za masomo, matumizi ya teknolojia na upatikanaji wa vyanzo mbadala vya fedha.
Mikakati hiyo imejadiliwa katika Kikao cha Mwaka cha Menejimenti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya wizara hiyo, kilichofunguliwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Profesa Carolyne Nombo, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda.
Profesa Nombo amesema kikao hicho kinalenga kutathmini utekelezaji wa bajeti ya mwaka uliopita, kupitia mafanikio na changamoto zilizojitokeza, pamoja na kuweka mikakati itakayowezesha sekta ya elimu kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Amesema mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa shughuli za wizara yametokana na usimamizi mzuri wa viongozi na ushirikiano wa taasisi zilizo chini ya wizara hiyo, licha ya changamoto mbalimbali zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa bajeti.
Kwa mujibu wa Profesa Nombo, wataalamu kutoka Tume ya Mipango wameshirikishwa katika kikao hicho ili kusaidia kuoanisha mipango ya sekta ya elimu na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Amesema utekelezaji wa dira hiyo unahitaji mfumo wa elimu unaozalisha wahitimu wenye maarifa na ujuzi unaokidhi mahitaji ya uchumi wa sasa na wa baadaye, hivyo kuna ulazima wa kufanya mapitio ya kozi na programu mbalimbali zinazotolewa katika ngazi zote za elimu.
Aidha, amesema mjadala unaoendelea kuhusu kozi zinazopaswa kuchaguliwa na wahitimu wa kidato cha sita umeonesha umuhimu wa sekta ya elimu kuendelea kupokea maoni ya wadau na kuyatumia kuboresha mitaala na programu za masomo ili ziendane na mahitaji ya soko la ajira.
Profesa Nombo amesisitiza pia matumizi ya Mfumo wa Taarifa za Usimamizi wa Elimu (ESMIS), akieleza kuwa takwimu sahihi ni msingi wa kupanga, kufanya maamuzi na kuboresha utoaji wa huduma za elimu.
Ameagiza taasisi zote kuhakikisha mifumo yao ya TEHAMA inaunganishwa na mfumo huo kwa kuzingatia maelekezo ya Serikali ya kuhakikisha mifumo ya umma inasomana.
Pia amewataka viongozi wa taasisi kuongeza ushirikiano na sekta binafsi katika uwekezaji wa elimu na kubuni njia mbadala za kuongeza mapato, akibainisha kuwa hatua hiyo itasaidia kuimarisha utoaji wa huduma hata katika kipindi ambacho bajeti za Serikali zinakabiliwa na changamoto.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Daniel Mushi, aliwataka watendaji wa wizara na taasisi zake kuendelea kutangaza mafanikio yanayopatikana kupitia miradi na programu mbalimbali za Serikali ili wananchi waendelee kufahamu hatua zinazochukuliwa kuboresha sekta ya elimu.
Washiriki wa kikao hicho walijadili mada mbalimbali, ikiwemo nafasi ya elimu, sayansi na teknolojia katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, matumizi ya mifumo ya TEHAMA na ESMIS, Mpango Mkakati wa Wizara wa mwaka 2026/27 hadi 2030/31, pamoja na utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2026/27.
MWISHO.





.jpeg)
