Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
WAKAGUZI WATAKIWA KUSIMAMIA UBORA, USALAMA WA MAZAO YA UVUVI

WAKAGUZI WATAKIWA KUSIMAMIA UBORA, USALAMA WA MAZAO YA UVUVI

 

Na Fadhili Abdallah,Kigoma 

Wasimamizi wa mazao ya uvuvi nchini wametakiwa kuongeza umakini katika kusimamia ubora na usalama wa samaki, dagaa na mazao mengine ya uvuvi ili kuhakikisha bidhaa zinazouzwa ndani na nje ya nchi zinakidhi viwango vya kimataifa.

Mkurugenzi Msaidizi wa Uvuvi nchini,Christian Nzowa ametoa wito huo wakati wa mafunzo ya siku tano kwa  wakaguzi na wasimamizi wa mazao ya uvuvi kutoka mikoa saba ya Tanzania bara na Zanzibar ambapo alisema kuwa  ubora na usalama wa mazao hayo ni nguzo muhimu katika sekta ya uvuvi nchini.

Nzowa alisema kuwa wakaguzi wanapaswa kusimamia kikamilifu hatua zote za mnyororo wa thamani wa mazao ya uvuvi kuanzia uvunaji, usafirishaji, uhifadhi, uchakataji hadi kufika sokoni ili kuhakikisha bidhaa zinabaki salama na zenye ubora unaokubalika ili kulinda afya za walaji, kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania kwenye masoko ya kimataifa na kukuza mchango wa sekta ya uvuvi katika uchumi wa taifa.

Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo Mtendaji Mkuu wa Wakala wa elimu ya mafunzo ya uvuvi (FETA),Dk. Semvua Mzighanyi alisema kuwa wakaguzi wa mazao ya uvuvi ndiyo nguzo muhimu inayochochea katika kuzingatia ubora na kutekeleza mpango wa kufuata mnyororo wa thamani.

Dk.Mzighanyi alisema kuwa kadri ubora na usalama wa mazao ya uvuvi unavyoongezeka ndivyo fursa ya kuyauza nje inavyokuwa kubwa katika kupanua masoko ya kimataifa, kuchochea ongezeko la fedha za kigeni kupitia mazao ya uchumi na kuchangia ukuaji wa pato la Taifa.

Kwa upande wake Mratibu wa mradi wa uboreshaji wa sekta ya uvuvi na kuongeza mazao ya uvuvi katika ziwa Tanganyika (FISH$ACP), Hashim Muumin alisema kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi huo ili kuwezesha mazao ya uvuvi kuwa na ubora wake kutoka ziwani hadi kufikia mlaji wa mwisho ambapo hatua mbalimbali zimechukuliwa ikiwemo mafunzo hayo kwa wakaguzi wa mazao ya uvuvi. 

mwisho

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3