Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
l MAVUNDE AAGIZA USIMAMIZI WA SHERIA KUONGEZA USHIRIKI WA WATANZANIA MIGODINIl

l MAVUNDE AAGIZA USIMAMIZI WA SHERIA KUONGEZA USHIRIKI WA WATANZANIA MIGODINIl

NA CHAUSIKU SAID

MATUKIO DAIMA MWANZA.

MWANZA, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, ameagiza usimamizi madhubuti wa Sheria ya Madini na kanuni zake ili kuhakikisha Watanzania wanapata nafasi kubwa zaidi katika kutoa bidhaa na huduma zinazotumika kwenye migodi nchini.

Waziri Mavunde amesema Serikali inalenga kuona asilimia 90 ya bidhaa na huduma zinazotumika katika migodi zikizalishwa na kutolewa na Watanzania, hatua inayolenga kuongeza manufaa ya Sekta ya Madini kwa wananchi na kukuza uchumi wa ndani.


Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Jukwaa la Tano la Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini lililofanyika Mwanza, Waziri Mavunde amesema utekelezaji wa sheria hizo ni muhimu katika kuhakikisha fursa zinazotokana na ukuaji wa sekta hiyo zinawanufaisha Watanzania

“Serikali inatarajia kuona asilimia 90 ya bidhaa na huduma zinazotumika katika migodi zikizalishwa na kutolewa na Watanzania, hili linahitaji usimamizi madhubuti wa sheria, pamoja na Watanzania kujiandaa kutumia fursa zinazopatikana katika Sekta ya Madini.”

Amesema ongezeko la uwekezaji katika Sekta ya Madini na matarajio ya kuanzishwa kwa migodi mipya yanafungua fursa zaidi kwa watoa huduma wa ndani, hivyo wanapaswa kujiandaa kwa kuongeza ubora wa bidhaa na huduma zao.


Waziri Mavunde pia amewataka wawekezaji katika sekta hiyo kuzingatia sheria na kanuni za nchi ili kuhakikisha uwekezaji wao unakuwa na tija kwa Taifa.

Amesema maboresho yaliyofanyika katika sekta ya madini yameongeza ushiriki wa Watanzania, ambapo kwa sasa ununuzi wa bidhaa na huduma katika sekta hiyo umefikia Shilingi trilioni 5.1 kwa mwaka.

Aidha, amesema Sekta ya Madini imezalisha ajira rasmi 20,421, huku ajira 16,695 zikishikiliwa na Watanzania, ikiwa ni sehemu ya mafanikio ya kuongeza ushiriki wa wananchi katika sekta hiyo


Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba, amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji huku ikiwasisitiza watoa huduma migodini kuzingatia ubora, weledi na uadilifu.

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dkt. Janet Lekashingo, amesema Jukwaa la Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini limekuwa na manufaa makubwa katika kuchochea ushiriki wa Watanzania katika sekta hiyo.

Amesema mafanikio hayo yanaonekana kupitia ongezeko la uwasilishaji wa mipango ya ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini, kutoka mipango 51 mwaka 2018 hadi kufikia mipango 1,312 mwaka 2025.


Naye Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Amir Mkalipa, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, ameipongeza Wizara ya Madini kwa juhudi zake za kuendelea kuvutia uwekezaji katika Mkoa wa Mwanza.

Amesema uwekezaji huo umechangia kuanzishwa kwa Mgodi wa Dhahabu wa Sotta Mining, ambao unatarajiwa kutoa ajira 1,500 utakapoanza uzalishaji.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3