Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
HUDUMA ZA AFYA KWA WOTE KUPUNGUZA GHARAMA ZA MATIBABU

HUDUMA ZA AFYA KWA WOTE KUPUNGUZA GHARAMA ZA MATIBABU

 


Na Hamida Ramadhan, Matukio

Daima Media Dodoma

SERIKALI imesema utekelezaji wa mfumo wa Huduma za Afya kwa Wote pamoja na kuanzishwa kwa mfuko maalumu wa kuchangia matibabu ya wananchi utasaidia kupunguza mzigo wa gharama za matibabu, hususan kwa wananchi wanaohitaji huduma za kibingwa.


Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, wakati wa ziara yake katika Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) na Soko la Machinga jijini Dodoma.


Msigwa amesema mfuko huo tayari umewezesha watoto wengi kunufaika na huduma za kibingwa, ikiwemo upandikizaji wa uloto, huku akisisitiza kuwa mfumo wa Huduma za Afya kwa Wote ndio suluhisho la kudumu la kupunguza gharama za matibabu kwa wananchi.

Akiwa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Msigwa alikagua utoaji wa huduma na kujionea ujenzi wa kituo cha mionzi kinachojengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 10.


Amesema Serikali imeendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya afya kupitia fedha za maendeleo zinazotekelezwa na TAMISEMI.


Kwa mujibu wa Msigwa, Serikali imejenga majengo 87 ya huduma za dharura, majengo 30 ya wagonjwa mahututi (ICU), vituo viwili vya magonjwa ya milipuko, mitambo 21 ya kuzalisha hewa tiba, nyumba 432 za watumishi wa afya na kununua magari 382 ya kubebea wagonjwa.


Amesema tangu mwaka 2021 idadi ya vituo vya kutolea huduma za afya imeongezeka kwa kiwango kikubwa, ambapo zahanati zimeongezeka kutoka zaidi ya 7,000 hadi zaidi ya 8,000, huku hospitali zikiongezeka kutoka 444 hadi 475.


Aidha, amesema Serikali imeongeza upatikanaji wa dawa kupitia Bohari ya Dawa (MSD) kwa gharama ya shilingi bilioni 242.7, hatua iliyosaidia kiwango cha upatikanaji wa dawa kufikia asilimia 88.8.


"Kwa sasa dawa zipo. Zisipopatikana sehemu yoyote huo ni uzembe wa usimamizi, siyo kwamba Serikali haijanunua dawa," amesema Msigwa.


Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuimarisha viwanda vya dawa nchini kupitia kikosi kazi maalumu kwa lengo la kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2030 angalau asilimia 50 ya dawa zinazotumika nchini zinazalishwa ndani ya Tanzania.


Akizungumzia Hospitali ya Benjamin Mkapa, Msigwa amesema Serikali imeendelea kuiimarisha hospitali hiyo kuwa kituo cha huduma za kibingwa na kibingwa bobezi kupitia uwekezaji katika majengo ya kisasa, vifaa tiba, mifumo ya TEHAMA na kuongeza wataalamu pamoja na watumishi.


Amesema hospitali hiyo imeongezewa watumishi 1,076, inatoa huduma 17 za kibingwa bobezi na imeanza kupokea wagonjwa kutoka nje ya nchi, hatua inayochochea ukuaji wa utalii wa matibabu nchini.


Aidha, amesema Tanzania kwa sasa ina madaktari bingwa 3,225 na madaktari bingwa bobezi 332, huku Hospitali ya Benjamin Mkapa ikiwa na madaktari bingwa bobezi 30.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3