GST YAENDELEA KUTOA ELIMU KWA WACHIMBAJI ILI KUBORESHA UZALISHAJI.
NA CHAUSIKU SAID
MATUKIO DAIMA MWANZA.
Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania, GST, imeeleza kuwa inaendelea kutoa elimu kwa wachimbaji wa madini nchini ili kuboresha ufanisi katika shughuli za utafutaji, uchimbaji na uchenjuaji wa madini.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Huduma za Kijiolojia wa GST, Alex Rutagwelela wakati akizungumza na waandishi wa habari katika banda la taasisi hiyo kwenye Jukwaa la Tano la Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini.
Rutagwelela amesema elimu inayotolewa na GST imekuwa na mchango mkubwa katika kubadilisha uelewa wa wachimbaji ambao sasa wameanza kufanya kazi kwa kufuata utaratibu wa kitaalam.
“Hali hiyo imeleta tija kubwa katika uzalishaji wa madini nchini. Wachimbaji sasa wanajua namna sahihi ya kufanya kazi zao,” amesema.
Ameongeza kuwa utafiti uliofanywa na taasisi hiyo umeonesha kuwepo kwa madini katika maeneo mengi hapa nchini hivyo ni muhimu kutumia teknolojia na mbinu bora katika shughuli za uchimbaji na utafiti ili kuhakikisha uhakika wa matokeo.
Aidha, amebainisha kuwa shughuli za utafiti katika sekta ya madini zinaendelea kufanyika kwa kiwango kikubwa ili kutoa taarifa sahihi kwa wachimbaji na wawekezaji.

.jpeg)
.jpeg)