BALOZI SIRRO ATAKA WAHAMIAJI HARAMU KIGOMA WABANWE
Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Balozi Simon Sirro amezitaka mamlaka za serikali za mitaa mkoani Kigoma kuendelea kuhimiza matumizi ya daftari la wakazi kwa viongozi wa vitongoji, vijiji na Mitaa ili kukabiliana na wimbi kubwa la wahamiaji haramu linaloingia mkoani humo kutoka nchi jirani .
Agizo hilo limekija kufuatia kuendelea kuwepo kwa idadi kubwa ya wakazi wasio raia wa Tanzania wanaoendela kuingia, kuishi na kufanya kazi mkoani Kigoma bila kufuata taratibu za kisheria za uhamiaji.
Balozi Sirro ametoa agizo hilo alipozungumza kwa nyakati tofauti kwenye vikao vya mabaraza ya Madiwani wa Halmashauri za mkoa wa Kigoma ambapo amewataka madiwani kushirikiana na viongozi wa vijiji au mitaa kuwafichua raia wa kigeni wanaoishi katika maeneo yao kinyume na Sheria za nchi.
Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa serikali kupitia vyombo vyake vya ulinzi na usalama vitaendelea kuchukua hatua ya kuendesha misako kuwakamata raia wa kigeni wanaoishi mkoani humo kinyume cha sheria lakini pia kuwachukulia hatua watu wote wanaoishi na kuwafanyisha kazi raia wa kigeni bila kufuata sheria.
Mwisho.


