CHAD YATANGAZA KUJITOA ICC
Chad imekuwa nchi ya hivi karibuni kutangaza mipango ya kujitoa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) huku nchi hiyo ikidai kwamba kati ya mashauri 13 yaliyochunguzwa tangu mahakama hiyo kuanza kufanya kazi mwaka 2002, tisa yanahusu mataifa ya Afrika.
Chad inajiunga na orodha ya mataifa mengi yanayoituhumu mahakama hiyo ya ICC kwa ubaguzi, huku ikizitaka nchi za Afrika kuimarisha mifumo yao ya sheria ya ndani badala ya kutegemea mahakama za Magharibi.
Kwa mujibu wa serikali ya Chad ni kwamba mahakama hiyo ina ubaguzi dhidi ya mataifa ya Afrika. Burkina Faso, Mali na Niger nazo pia zimeanza mchakato wa kujitoa kutoka Mahakama ya ICC, ambayo inawashtaki watu binafsi kwa makosa ya hatia za kivita na makosa dhidi ya binadamu.
Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa umesema uamuzi wa Venezuela kujitoa kutoka Mahakama ya ICC wiki iliyopita unatia wasiwasi mkubwa na utazidisha utamaduni wa kutoadhibiwa kwa ukiukaji wa haki za binadamu. Maafisa wa Venezuela walitangaza kujitoa ICC huku wakidai mahakama hiyo ina ubaguzi wa kijiografia.