WANAOTUMIA MIKOPO KINYUME NA MALENGO WANAKWAMISHA MAREJESHO
Na Fadhili Abdallah,Kigoma
IMEELEZWA kuwa Wajasiliamali wasiofuata malengo na mikataba ya mikopo wanayochukua kutoka mapato ya ndani ya halmashauri wanakwamisha utoaji wa mikopo kwa wajasiliamali wengine kwa kushindwa kurejesha mikopo hiyo kwa wakati.
Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Lawi Kajanja alisema hayo wakati akifungua mafunzo ya uendeshaji biashara wenye tija, uwekaji wa hesabu za biashara na mipango mikakati ya biashara hizo kwa wajasiliamali kutoka vikundi 30 vya manispaa ya Kigoma Ujiji ambavyo vimekoposhwa kiasi cha shilingi milioni 362.5 kutoka mapato ya ndani ya halmashauri hiyo.
Kajanja alisema kuwa mikopo hii hutolewa kwa matarajio kwamba itatumika kwa malengo yaliyokusudiwa ili iweze kuleta matokeo chanya kwa mkopaji na jamii kwa ujumla ambapo hata hivyo baadhi ya wajasiriamali huamua kutumia mikopo hiyo katika shughuli zisizohusiana na malengo waliyoainisha wakati wa kuomba mkopo. matumizi mabaya ya fedha jambo linalosababisha biashara kushindwa kukua kama na hivyo kuathiri uwezo wa mkopaji kurejesha mkopo kwa wakati.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa kutorejeshwa kwa mikopo hiyo kwa wakati kunapunguza mzunguko wa fedha katika mfuko wa mikopo wa halmashauri hivyo kusababisha halmashauri kushindwa kutoa mikopo mipya kwa wakati kwa waombaji wengine wanaohitaji mtaji wa kuanzisha au kupanua biashara zao.
Awali Kaimu Afisa Maendeleo ya jamii wa halmashauri ya manispaa ya Kigoma Ujiji, jabiri Majira alisema kuwa jumla ya mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 326.5 imetolewa kwenye robo ya tatu ya halmashauri hiyo ya manispaa ya Kigoma Ujijina kunufaisha vikundi 30 kati yake vikiwemo vikundi 10 vywa vijana, wanawake vikundi 16 na makundi maalum vikundi vinne.
Majira alisema kuwa kutolewa kwa mikopo hiyo kunaifanya halmashauri hiyo kuwa imeshatoa kiasi cha shilingi Bilioni 1.1 ambapo hapo awali Zaidi ya shilingi milioni 800 zilikuwa zimeshatolewa kuanzia mwezi julai mwaka jana hadi kufikia sasa na hali ya urejeshaji ni nzuri na biashara nyingi za wajasiliamali zimeimarika.
Kwa upande wake Meneja biashara wa benki ya CRDB tawi la Kigoma,Victor Komba aliwakumbusha wajasiliamali kufuata maandiko ya miradi yao na mikataba wanayoingia na taasisi za fedha wanapochukua mikopo kinyume chake watashindwa kurejesha mikopo na kuzuia watu wengine kupata mikopo hiyo.
Mwisho.



.jpeg)