MTAFIKOLO AZIDI KUCHANJA MBUGA UBUNGE ISIMANI
NA MATUKIO DAIMA MEDIA
Mgombea wa Ubunge wa Jimbo la Ismani kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Emmanuela Mtatifikolo ameendelea kuchanja mbuga kusaka kura kwa wananchi wa jimbo la Isimani kwa kugusa mahitaji yao.
Katika kampeni zake katika Kata ya Kihorogota, Tarafa ya Ismani, wananchi wameonesha kumkubali zaidi mgombea huyo kutokana na sera za CCM zinazogusa maisha yao ukilinganisha na vyama vingine ambavyo wagombea wake wamekuwa wakibeza kazi zilizofanywa na serikali iliyopo madarakan.
Akiwa kwenye mikutano yake ya Kampeni Mtatifikolo amewaomba wananchi wote kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi mdogo wa jimbo hilo utakaofanyika Juni 1, 2026.
Katika mikutano hiyo ya kampeni, Emmanuela Mtatifikolo aliwasilisha sera zake na kueleza dhamira yake ya kuendeleza jitihada za maendeleo katika Jimbo la Ismani endapo atachaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo.
Mgombea huyo alisindikizwa na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Taifa, Mary Chatanda, Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Iringa, Eng. Fatma Rembo, pamoja na viongozi wa CCM Wilaya ya Iringa Vijijini wakiongozwa na Mwenyekiti wa Wilaya, Constantino Kihwele.
Akizungumza katika mikutano hiyo, Eng. Fatma Rembo aliwaomba wananchi wa Ismani kumpigia kura za kishindo Emmanuela Mtatifikolo ili kuendelea kuimarisha maendeleo na kuhakikisha jimbo hilo linapata uwakilishi madhubuti bungeni.
Uchaguzi mdogo wa Jimbo la Ismani unafanyika kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, William Lukuvi. Wananchi wa jimbo hilo wanatarajiwa kuchagua mbunge mpya katika uchaguzi utakaofanyika Juni 1, 2026.


