RC MTAKA ATAKA VIONGOZI WA DINI KUONGEZA JITIHADA KUWANUSURU WANANCHI KIROHO
Mkuu wa Mkoa wa Njombe Anthony Mtaka amesema jitihada za viongozi wa dini katika kuifikia jamii na kuhubiri neno la Mungu ili jamii iweze kubadilika na kutenda mema na kuacha maovu zinapaswa kuungwa mkono na kila Mtanzania.
Katika hafla ya chakula Cha mchana iliyoandaliwa nyumbani kwake yenye lengo la kuwapongeza viongozi wa kanisa la Waadventist Wasabato Tanzania ambao waliweka kambi ya mwezi mmoja kuhubiri neno la mungu na kutoa huduma za kitabibu kwa wananchi Mtaka amesema kazi Kubwa imefanyika katika kuwaweka sawa wananchi kiroho.Akizungumza wakati wa kuwakaribisha viongozi wa kanisa la Waadventist Wasabato Tanzania nyanda za juu kusini na kaskazini waliofika katika hafla pamoja na waumini wao Mtaka amesema tukio la kambi ya maombezi ni kubwa na limekuwa likifuatiliwa na watu wengi kupitia vyombo mbalimbali vya habari vya ndani na nje ya nchi kwa lugha tofauti.
Amesema kupitia mkutano huo wa injili watu wamepata mafundisho mengi na shuhuda mbalimbali kutoka maeneo tofauti hapa nchini ikionyesha dhahiri kuwa mkutano huo umekuwa na tija kubwa kwa wananchi hasa mkoani Njombe.
Aidha Hafla hiyo imefanyika ili kuwashukuru viongozi wa kanisa la Waadventist Wasabato Tanzania kwa kutoa huduma ya maombezi pamoja na ile ya matibabu bure kwa wananchi wa mkoa huo.
Amesema kufuatia hafla hiyo wakaona waalike kwaya mbalimbali ikiwemo kwaya ya wasabato ya kurasini, kwaya ya Magomeni na Galilaya ya Kigamboni pamoja na kwaya za ndani ya mkoa ili kushiriki kufunga kambi ya maombezi ya kanisa la Waadventist Wasabato mkoani hapa.
Askofu wa Kanisa la Wadventisti Wasabato Tanzania Jimbo la Kusini Joseph Mgwabi amesema kukutana kwenye hafla hiyo katika kilele cha kuhitimisha mikutano mikubwa ya injili iliyofanyika katika mji wa Njombe iliyojulikana kama "Njombe Net Event 2026 Tumaini lenye baraka" awali walikuwa hawafahamiani lakini wanaondoka wakiwa wanafahamiana kupitia tukio hilo.
Mwenyekiti wa Kanisa la Wadventisti Wasabato Jimbo la Kaskazini Mchungaji David Mpwani amesema Mtaka ana mchango mkubwa katika kufanikisha mkutano huo wa injili kutikana na maamuzi yake ya kutaka mkutano kufanyika mkoani hapa.



