Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
*KRFA YACHORA RAMANI MPYA YA SOKA KILIMANJARO, YABANA MASHINDANO HOLELA*

*KRFA YACHORA RAMANI MPYA YA SOKA KILIMANJARO, YABANA MASHINDANO HOLELA*


Kwa ufupi:KRFA imepitisha maazimio ya kuimarisha maendeleo ya soka Kilimanjaro, yakiwemo kudhibiti mashindano holela (ndondo), kuzuia udanganyifu wa umri, kuibua vipaji na kuongeza waamuzi, katika mkutano mkuu wa kawaida uliofanyika Moshi


Moshi.Chama cha Soka Mkoa wa Kilimanjaro (KRFA) kimekuja na ramani mpya ya maendeleo ya soka mkoani humo baada ya kupitisha maazimio kadhaa yatakayobana mashindano holela, kuibua vipaji vya vijana na kuongeza idadi ya waamuzi.

Maazimio hayo yamepitishwa katika mkutano mkuu wa kawaida wa chama hicho uliofanyika Moshi, huku viongozi wakisisitiza kuwa muda wa kuendesha soka bila utaratibu umefikia mwisho.

Maazimio hayo yamepitishwa katika mkutano mkuu wa kawaida wa chama hicho uliofanyika katika ukumbi wa mkutano wa Chuo Kikuu Cha Ushirika Moshi, huku viongozi wakisisitiza kuwa muda wa kuendesha soka bila utaratibu umefikia mwisho.

Akizungumza leo Juni 1,2026 baada ya kikao hicho kilichofanyika  katika ukumbi wa mkutano wa Chuo Kikuu Cha Ushirika Moshi,Katibu wa KRFA Thabit Abdalla amesema kuanzia sasa waandaaji wote wa mashindano ndani ya Mkoa wa Kilimanjaro watalazimika kufuata taratibu rasmi za chama hicho kabla ya kupewa ruhusa ya kuendesha ligi au mashindano yoyote.

Amesema hatua hiyo imelenga kuondoa migogoro na changamoto ambazo zimekuwa zikijitokeza mara kwa mara kwenye mashindano yanayoanzishwa bila kufuata misingi ya soka.

“Sisi ndio wenye dhamana ya kusimamia mpira wa miguu ndani ya Mkoa wa Kilimanjaro. Tumekubaliana mashindano yote lazima yaanze ngazi ya wilaya, yapate kibali na baadaye yathibitishwe na mkoa,” amesema Thabit.

Aidha mkutano huo umeazimia kuhamasisha wananchi wa Kilimanjaro kuisapoti Polisi Tanzania katika harakati za kupanda Ligi Kuu Bara msimu huu, huku Enduimet ya first league ikipewa msukumo wa kufanya vizuri kwenda Championship.

“Mkoa wa Kilimanjaro unahitaji kuona timu zake zinapiga hatua. Polisi Tanzania lazima tupambane irudi Ligi Kuu,” amesema Thabit.

Mbali na kudhibiti mashindano holela, KRFA pia imepitisha mpango wa kuanzisha vituo vya kukuza vipaji vya vijana katika wilaya za Moshi Manispaa, Siha na Hai ili kuongeza ushindani wa soka la vijana.

Katika hatua nyingine, chama hicho kimeweka mkakati wa kuzalisha waamuzi wapya kwa kila wilaya, huku kila chama cha wilaya kikitakiwa kuwasilisha ripoti ya maendeleo ya waamuzi katika mkutano mkuu ujao.

Mwenyekiti wa Waamuzi Mkoa wa Kilimanjaro, Godbless Kimaro amesema changamoto kubwa iliyopo kwenye soka la Tanzania ni uelewa mdogo wa tafsiri sahihi ya sheria za mchezo.

Amesema KRFA imeanza programu maalumu za kuwafundisha waamuzi kuanzia ngazi za shule ili kujenga kizazi kipya cha waamuzi wenye uwezo wa kuchezesha mechi za kitaifa na kimataifa.

“Tunataka watoto waanze mapema kujifunza sheria za mpira wa miguu. Hii itatusaidia kupata waamuzi bora wa baadaye na kupunguza malalamiko yanayoendelea kwenye ligi,” amesema Kimaro.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ufundi wa KRFA, Issa Rugaza amesema chama hicho pia kitaanza kusimamia kwa ukali suala la umri katika mashindano ya vijana ili kulinda vipaji vya kweli.

Rugaza amesema baadhi ya mashindano yamekuwa yakiharibiwa na matumizi ya wachezaji waliovuka umri, hali inayowanyima nafasi vijana wenye vipaji halisi kuonekana.

“Hatuwezi kujenga soka la baadaye kwa kutumia njia za mkato. Tunahitaji watoto wenye umri sahihi waendelezwe ili Mkoa wa Kilimanjaro upate wachezaji wa ushindani miaka ijayo,” amesema Rugaza.

Mbali na maazimio hayo, KRFA pia imezindua mashindano ya vijana yatakayojulikana kama Kilimanjaro Utalii Super Cup, yatakayolenga kutangaza vivutio vya utalii kupitia michezo kuelekea AFCON 2027.

Akizungumza katika mkutano huo Mwenyekiti wa KRFA, Isaac Munisi amesema mafanikio ya soka la Kilimanjaro hayatapatikana bila kuimarisha ligi za kimfumo na kuheshimu katiba pamoja na kanuni za mchezo huo kuanzia ngazi za wilaya.

Munisi amesema bado baadhi ya wilaya zimekuwa zikikumbwa na changamoto ya kushindwa kuendesha ligi zao, huku akizitaka kuacha kutegemea zaidi mashindano ya ndondo na badala yake kuwekeza nguvu kwenye ligi rasmi zinazotambulika kikatiba.

“Tuache kuangalia ndondo kuliko ligi za kimfumo. Tukisimamia katiba na kanuni zetu vizuri, tutapata ubora wa ligi na maendeleo ya mpira wetu,” amesema Munisi.
Amesema KRFA pia imeweka mkazo mkubwa kwenye maendeleo ya vijana, huku akizitaka wilaya zote kuanzisha vituo vya vijana vitakavyokuwa vikifanya mazoezi angalau mara mbili kwa wiki chini ya walimu wanaotambulika rasmi na chama cha makocha.

“Kipaumbele chetu kikubwa sasa ni vijana. Kila wilaya iwe na kituo yake cha  vijana, walimu wapo, waamuzi wapo, sasa tuweke nguvu kwenye malezi ya vipaji,” amesema Munisi.

Mwisho.



Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3