Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
MAFUNZO YA ITIKADI NA UENEZI KUJENGA KIZAZI KIPYA CHA VIONGOZI CCM ILEMELA.

MAFUNZO YA ITIKADI NA UENEZI KUJENGA KIZAZI KIPYA CHA VIONGOZI CCM ILEMELA.

 

NA CHAUSIKU SAID

MATUKIO DAIMA MWANZA 

MWANZA, Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ilemela kimesema mafunzo ya siasa, itikadi na uenezi yanayotolewa kwa wanachama na makada wake ni mkakati wa kuandaa kizazi kipya cha viongozi wenye uelewa wa misingi, katiba na taratibu za chama.

Kauli hiyo imetolewa jana juni 4, 2026 na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Wilaya ya Ilemela, Salumu Mtaturu, wakati wa kufunga mafunzo ya siasa, itikadi na uenezi yaliyofanyika katika Kata ya Kahama Mkoani Mwanza.

Mtaturu alisema chama kimebaini kuwa wanachama wengi hujiunga na CCM kwa sababu mbalimbali ikiwemo kurithi uanachama kutoka kwa familia zao, kushawishiwa na watu waliopo ndani ya chama au kujiunga kwa hiari yao, hali inayosababisha baadhi yao kutokuwa na uelewa wa kutosha kuhusu historia na misingi ya chama hicho.

Alisema mafunzo hayo yanalenga kuziba pengo hilo kwa kuwajengea wanachama uwezo wa kuelewa itikadi, maadili na wajibu wao ndani ya chama ili waweze kukitetea na kukiongoza kwa ufanisi siku zijazo.

“Tunataka wanachama wetu waelewe kwa kina chama walichomo, wajue misingi yake na wawe na uwezo wa kusimamia kile wanachokiamini kwa uelewa sahihi. Hii ni hatua muhimu katika kuandaa viongozi wa kesho,” Alisema Mtaturu.

Aidha, amewataka wahitimu wa mafunzo hayo kuwa mabalozi wa elimu kwa wanachama wengine na kuendelea kuzingatia misingi iliyoasisiwa na waasisi wa CCM.

Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Esther Sengelema, amesema elimu aliyopata itamsaidia kuboresha utendaji wake ndani ya chama, hususani katika masuala ya itifaki na uendeshaji wa vikao.

“Tulikuwa tunakosa uelewa wa baadhi ya taratibu za chama, lakini kupitia mafunzo haya tumepata maarifa yatakayotuongoza katika utekelezaji wa majukumu yetu,” alisema.

Kwa upande wake, Katibu wa CCM Kata ya Kahama, ambaye pia ni mhitimu wa mafunzo hayo Petro shimbe, alisema mafunzo hayo yameongeza uelewa wa wanachama kuhusu katiba, kanuni na miongozo ya chama na kuwapa wajibu wa kuifikisha elimu hiyo kwa wanachama wengine.

Naye mkufunzi wa mafunzo hayo, Wakumela Mlongo, alisema mafunzo yalianza Mei 22 na kuhitimishwa Juni 4 mwaka huu, huku idadi ya washiriki ikiongezeka kutoka wanane hadi kufikia takribani 30.

Alieleza kuwa mafunzo hayo yatasaidia kukuza uzalendo, mshikamano na uelewa wa itifaki za chama, huku yakichangia kujenga CCM yenye viongozi na wanachama wanaozingatia katiba, kanuni na miongozo ya chama.

Kwa mujibu wa waandaaji, wahitimu wa mafunzo hayo wanatarajiwa kuwa chachu ya kueneza elimu ya siasa na itikadi katika maeneo yao, hatua inayolenga kuimarisha uimara wa chama kuanzia ngazi za msingi hadi taifa.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3