Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
WALIMU KUSHINDANIA MAMILIONI KATIKA SHINDANO LA UBUNIFU WA UFUNDISHAJI

WALIMU KUSHINDANIA MAMILIONI KATIKA SHINDANO LA UBUNIFU WA UFUNDISHAJI

 


Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma


WALIMU  wa shule za awali, msingi na sekondari nchini wanatarajiwa kushindania zawadi za mamilioni ya shilingi katika Shindano la Kitaifa la Stadi za Ufundishaji litakalofanyika Juni 6, 2026, huku Serikali ikilenga kuhamasisha matumizi ya mbinu bora na shirikishi za ufundishaji darasani.


Akizungumza na waandishi wa habari leo, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir, amesema shindano hilo ni jukwaa muhimu la kuwatambua walimu wanaoonesha umahiri, ubunifu na uwezo wa kutumia mbinu zinazokuza ujifunzaji wenye tija kwa wanafunzi.



Amesema shindano hilo linasimamiwa na Wizara ya Elimu kwa kushirikiana na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) na ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Kitaifa wa Mafunzo Endelevu ya Walimu Kazini (MEWAKA), unaolenga kuboresha ubora wa elimu nchini.


Kwa mujibu wa Ameir, malengo ya shindano hilo ni pamoja na kuwatambua walimu wanaotumia mbinu shirikishi zinazokuza Stadi za Karne ya 21, kuimarisha upimaji na utoaji wa mrejesho kwa wanafunzi pamoja na kuwajengea uwezo wa kuandaa maudhui yatakayotumika kupitia Mfumo wa Kidijitali wa Ujifunzaji (LMS).





Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Profesa Carolyne Nombo, amesema walimu 3,153 walijisajili kushiriki katika mashindano ya mwaka huu kupitia mfumo wa National Teaching Skills Competition System (TSCS), huku walimu 1,263 wakikamilisha masharti ya ushiriki kwa kuwasilisha video za ufundishaji na maandalio ya masomo kwa ajili ya tathmini.


Amesema mashindano ya mwaka huu yanahusisha maeneo saba ambayo ni Kusoma kwa Darasa la Awali, Kiingereza kwa Darasa la Kwanza, Ufaraguzi wa Zana kwa Darasa la Pili pamoja na masomo ya Physics, Mathematics, Business Studies na Computer Science kwa walimu wa shule za sekondari.


Profesa Nombo amesema mshindi wa kwanza katika kila eneo la ushindani atajinyakulia Sh2.5 milioni, cheti cha pongezi, cheti cha ushindi na kompyuta mpakato, huku shule anayofundisha ikipata projekta.



Aidha, amesema video za washindi wote wa nafasi ya kwanza zitarekodiwa upya katika studio za TET na kupakiwa kwenye Mfumo wa Elimu wa Kidijitali (LMS) pamoja na kurushwa kupitia TET Soma Kwanza TV ili walimu wengine nchini wapate fursa ya kujifunza mbinu hizo bora za ufundishaji.


Shindano hilo linabeba kaulimbiu ya "Ufundishaji Bora, Taifa Imara", likitarajiwa kuwa chachu ya kuimarisha ubora wa elimu na matokeo ya ujifunzaji kwa wanafunzi nchini.







Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3