Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
BATILDA AONGOZA HARAMBEE BIL.25 YA KCMC MOYO, AKUSANYA MIL.100 TANGA

BATILDA AONGOZA HARAMBEE BIL.25 YA KCMC MOYO, AKUSANYA MIL.100 TANGA

 



NA AMINA SAIDI, MATUKIO DAIMA TANGA.


​MKUU wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Burian, amewataka wakazi wa mkoa huo na wadau wa maendeleo kujitokeza kwa wingi kuchangia ujenzi wa Taasisi ya Moyo katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC, mradi unaolenga kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi na kupunguza msongamano katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) jijini Dar es Salaam.


​Wito huo umetolewa  wakati Dkt. Batilda akiongoza harambee maalum ya kuchangia mradi huo, uliyofanyika katika viwanja vya Tanga Beach Resort. Katika harambee hiyo, zaidi ya Sh. milioni 100 zilichangwa hapo hapo na wadau wa maendeleo, huku wengine wakitoa ahadi za kuendelea kuchangia.


​Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Batilda alisisitiza kuwa kukamilika kwa hospitali hiyo kutakuwa ukombozi mkubwa kwa wakazi wa mikoa ya Kanda ya Kaskazini—Tanga, Kilimanjaro, Arusha, na Manyara—ambako changamoto ya magonjwa ya moyo imekuwa ikiongezeka kwa kasi.

​"Kanda ya Kaskazini pekee inachangia asilimia 60 ya wagonjwa wote wa moyo wanaotibiwa JKCI Dar es Salaam.


 "Hospitali hii ikikamilika, itasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza msongamano wa wagonjwa wanaokwenda JKCI na hata wale wanaolazimika kusafiri nje ya nchi kufuata matibabu," alisema Dkt. Batilda.


​ 

​Mkuu huyo wa mkoa alifafanua kuwa mradi huo mzima unagharimu Sh. bilioni 25, na hadi sasa kiasi cha Sh. bilioni 22 kimeshapatikana na kuwezesha ujenzi kufikia asilimia 40. Alibainisha kuwa kiasi kilichobaki cha Sh. bilioni 3 kitatumika maalum kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa.


​"Ndugu zangu, tumekuja hapa ili tuwe sehemu ya watu waliotoa mchango wa kuokoa maisha ya ndugu zetu.


 Niwaombe tuendelee kuhamasishana. Zoezi hili si la leo tu bali ni endelevu; kwa yeyote atakayeguswa kuchangia, milango ya ofisi ya Mkuu wa Mkoa iko wazi," alisisitiza.


​Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa KCMC, Profesa Gilead Masenga, alitahadharisha kuwa magonjwa yasiyoambukiza (NCDs) yamekuwa tishio kubwa na ndiyo yanayoongoza kwa kuathiri jamii kwa sasa.


​Profesa Masenga alifichua takwimu za kutisha akisema: "Hivi sasa katika Hospitali ya KCMC, kati ya wagonjwa 10 wanaoletwa kupata matibabu, wagonjwa 8 hadi 9 wanasumbuliwa na magonjwa yasiyoambukiza, yakiwemo shinikizo la juu la damu na kisukari."


 Profesa Masenga alisema KCMC iliazimia kuanzisha taasisi hiyo ili kutoa huduma za kibingwa kwa haraka, badala ya wagonjwa kusubiri kwenye foleni ndefu za rufaa.


​Aliongeza kuwa hospitali hiyo, ambayo ina uzoefu wa kutoa huduma za kibingwa kwa zaidi ya miaka 50, imeshajipanga vizuri upande wa rasilimali watu ili kuanza kazi mara moja ujenzi utakapokamilika.


​"Tayari tumeshawaandaa wataalamu wetu wa kutosha na tukawapeleka nje ya nchi kwa ajili ya masomo ya kibingwa ya magonjwa ya moyo.


 Hivi sasa wamesharudi na wapo tayari kwa kazi, tunachosubiri kwa sasa ni kukamilika kwa miundombinu ya ujenzi tu," alihitimisha Profesa Masenga.



Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3