WADAU WA ELIMU WASISITIZWA KUSHIRIKI KUIMARISHA ELIMU JUMUISHI TANZANIA
Na: Samwel Mpogole, Mbeya
Wakati juhudi za kuhakikisha kila mtoto anapata haki sawa ya elimu zikiendelea kupewa msukumo nchini, Mkuu wa Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya, Maulid Surumbu, amezitaka halmashauri nchini kuweka kipaumbele katika uanzishaji na uimarishaji wa Vituo vya Upimaji, Utambuzi na Rasilimali za Elimu kwa Watoto (ESRAC) ili kusaidia watoto wenye changamoto mbalimbali kupata huduma za elimu kwa wakati.
Sulumbu ametoa kauli hiyo wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kitaifa ya ujenzi na matumizi ya vituo vya ESRAC uliofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Mwenge, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Benno Malisa.
Amesema huduma za utambuzi wa mapema zina mchango mkubwa katika kujenga mfumo bora wa elimu jumuishi kwa kuwa huwasaidia watoto wenye mahitaji maalumu kutambuliwa mapema na kupatiwa msaada unaostahili kabla changamoto zao hazijawa kubwa zaidi.
“Watoto hawa wana haki sawa ya kupata elimu bora kama watoto wengine. Ni wajibu wa jamii, serikali na wadau kuhakikisha wanapata mazingira rafiki yatakayowasaidia kufikia ndoto zao,” amesema Sulumbu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa HakiElimu, Marry Ndaro, amesema mafanikio ya kampeni hiyo yanahitaji ushirikiano wa karibu kati ya serikali, wadau wa maendeleo pamoja na jamii ili kuhakikisha huduma za utambuzi na upimaji zinapatikana kwa watoto wengi zaidi nchini.
Ndaro amesema vituo vya ESRAC vina umuhimu mkubwa katika kubaini mapema changamoto za watoto ikiwemo ulemavu na mahitaji maalumu ya kujifunza, hatua inayosaidia kuongeza ufanisi wa ujifunzaji na maendeleo yao kwa ujumla.
Naye mzazi wa mtoto mwenye mahitaji maalumu, Angela Fares, amesema msaada alioupata kupitia Child Support Tanzania umemwezesha mtoto wake mwenye ulemavu wa akili kupata haki yake ya elimu na kuanza kuona mabadiliko chanya katika maisha yake.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Child Support Tanzania, Noela Msuya, amesema kuwa elimu jumuishi ni nguzo muhimu katika kuhakikisha hakuna mtoto anayebaki nyuma katika mfumo wa elimu. Amesema shirika hilo linaendelea kushirikiana na serikali pamoja na wadau mbalimbali katika kuimarisha huduma za utambuzi wa mapema kwa watoto wenye mahitaji maalumu kupitia vituo vya ESRAC, ili kuwasaidia kupata msaada stahiki kwa wakati.
Uzinduzi huo umebebwa na kauli mbiu isemayo; “Utambuzi wa Mapema, Msingi wa Elimu Jumuishi na Bora kwa Watoto Wote,” ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhamasisha jamii kutambua umuhimu wa elimu jumuishi na huduma za mapema kwa watoto wenye changamoto mbalimbali.



