Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
MSHTAKIWA WA TATU AJUMUISHWA KATIKA KESI YA MAUAJI YA LAS VEGAS BAR

MSHTAKIWA WA TATU AJUMUISHWA KATIKA KESI YA MAUAJI YA LAS VEGAS BAR

 


NA CHAUSIKU SAID -MATUKIO DAIMA MWANZA.


Mahakama ya Wilaya ya Ilemela imepokea hati iliyorekebishwa ya mashtaka katika kesi ya mauaji ya Mzafuru Faisal Yunusu, hatua iliyosababisha kuongezwa kwa mshtakiwa wa tatu anayehusishwa na tukio hilo lililotokea katika baa ya Las Vegas, eneo la Kona ya Bwiru wilayani Ilemela.


Mshtakiwa mpya, Benson John (19), mkazi wa Nyakabungo, Kata ya Isamilo wilayani Nyamagana na anayefanya kazi ya ulinzi (baunsa), amefikishwa mahakamani Juni 3, 2026 na kuunganishwa rasmi katika shauri la jinai namba 10492 la mwaka 2026 linalowakabili watuhumiwa wa mauaji hayo.


Wakili wa Serikali, Mwanahawa Changale, akiungwa mkono na Clara Muhando, aliwasilisha ombi la kupokelewa kwa hati mpya ya mashtaka chini ya kifungu cha 251 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2023, ili kumjumuisha mtuhumiwa huyo katika shauri hilo.


Kufuatia hatua hiyo, idadi ya washtakiwa katika kesi hiyo imeongezeka na kufikia watatu. Wengine ni Yohana Paul Peter (22), ambaye ni baunsa wa eneo hilo, na Hamis Juma Mussa (27), mfanyakazi wa usafi.



Washtakiwa hao walifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Ilemela, Juma Opudo, aliyekuwa akikaimu kwa niaba ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Christian Mwalimu, ambaye ndiye anayesimamia shauri hilo.


Upande wa mashtaka ulidai kuwa Februari 5, 2026, washtakiwa hao walimuua Mzafuru Faisal Yunusu katika baa ya Las Vegas kwa kumpiga, kitendo kinachodaiwa kuwa kinyume na vifungu vya 196 na 197 vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu.


Hata hivyo, washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu chochote kuhusu tuhuma hizo kwa kuwa Mahakama ya Wilaya haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji, bali huzitaja kabla ya kupelekwa Mahakama Kuu kwa hatua zaidi za kisheria.


Hakimu Opudo alieleza kuwa kwa kuwa kosa la mauaji halina dhamana, washtakiwa wataendelea kubaki mahabusu hadi upelelezi wa shauri hilo utakapokamilika.


Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 17, 2026, kwa ajili ya kutajwa tena, huku washtakiwa wote watatu wakirejeshwa rumande kusubiri hatua zinazofuata za kisheria.



Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3