UMALITA KUFUNGUA FURSA KWA MAMA LISHE NA BABA LISHE KIGOMA
Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Mama lishe na baba lishe wanaofanya shughuli ya kuuza chakula kwenye mahoteli na migahawa wametakiwa kujiunga pamoja kwenye vikundi kupitia Umoja wa Mama Lishe Tanzania (UMALITA) ili waweze kunufaika na fursa zinazotolewa na serikali na wadau mbalimbali zinazolenga kuboresha maisha yao na kukuza biashara zao.
Katibu Mwenezi wa Taifa Mhamasishaji wa UMALITA,Rehema Sule alisema hayo akianza ziara mkoani Kigoma kuhamasisha mama lishe kujiunga na umoja huo sambamba na kusimamia chaguzi za umoja huo kwa ngazi za wilayana mkoa Kigoma ambapo alisema kuwa umoja huo umeanzishwa kwa lengo la kuwaunganisha wafanyabiashara hao wadogo na kuwawezesha kupata nguvu ya pamoja katika kutatua changamoto zinazowakabili katika shughuli zao za kila siku.
Sule alisema kuwa kupitia umoja huo mama lishe watapata fursa ya kutangaza huduma zao na kupanua wigo wa soko la bidhaa wanazouza. kupata masoko mapya, kushiriki maonesho ya biashara na kuunganishwa na taasisi mbalimbali zinazohitaji huduma za chakula katika mikutano, semina na matukio mengine.
Alisema kuwa tayari Rais Samia Suluhu Hassan ameweka Baraka yake kwa umoja huo ambapo viongozi watatumia nafasi yao Katika kuimarisha uchumi wa wanachama, kushirikiana na taasisi za kifedha kuwezesha upatikanaji wa mikopo yenye masharti nafuu Ili huwasaidia mama lishe kuongeza mtaji, kuboresha maeneo ya biashara na kununua vifaa vya kisasa vinavyoongeza ufanisi wa kazi zao.
Mhamasishaji huyo alisema kuwa umoja kwa kushirikianana wadau mbalimbali utatoa mafunzo ya ujasiriamali, usimamizi wa fedha, usalama wa chakula na huduma bora kwa wateja. Mafunzo ambayo yameelezwa kuwa yatawajengea uwezo wanachama kuendesha biashara zao kwa weledi zaidi na kuongeza ushindani katika soko.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa UMALITA mkoa Kigoma, Revina Kachira alisema kuwa kwa sasa Mama lishe na Baba lishe mkoa Kigoma wanafanya kazi kila mtu kivyake wakiwa na ushindani lakini kuwepo kwa umoja huo kutawezesha kuwaweka pamoja kuzungumzia changamoto zao na namna ya kupata pesa za kuimarisha shughuli zao.
Akizungumza wakati Kiongozi huyo wa UMALITA Taifa alipofikia ofisini kwake kujitambulisha Afisa Maendeleo ya jamii katika sekretariet ya mkoa Kigoma anayeshughulikia makundi maalum, Minza Edward alisema kuwa kuwepo kwa makundi maalum ambayo yameungana na kuwa na utambulisho rasmi yanawapa nafasi nzuri ya kuwafikia kwa haraka zinapotokea fursa mbalimbali ikiwemo mafunzo ,uwezeshaji, mikopo na hata baadhi ya makundi yanapohitajika kwa shughuli maalum.




