Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
*TANZANIA NA URUSI KUSHIRIKIANA KATIKA KUENDELEZA UTAFITI WA MADINI*

*TANZANIA NA URUSI KUSHIRIKIANA KATIKA KUENDELEZA UTAFITI WA MADINI*

Ni ushirikiano baina ya Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania(GST) na Chuo Kikuu cha Urusi

Rais Samia afungua fursa zaidi kwa wawekezaji wa madini kutoka Urusi

Madini ya Bauxite yapewa kipaumbele kwenye utafiti

*Moscow, Urusi 🇷đŸ‡ē *

Akishiriki ziara rasmi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Urusi, leo tarehe 05 Juni, 2026 Jijini Moscow, Waziri wa Madini, *Mh. Anthony Peter Mavunde (Mb)* amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Serikali ya Urusi kwenye sekta ya madini ukiongozwa na Naibu Waziri wa Maliasili(Madini) na Mazingira wa Shirikisho la Urusi, *Mh. Tetenkin Dmitry Dmitrievich*.

Katika mazungumzo hayo, Waziri Mavunde alieleza namna sekta ya madini inavyozidi kukua na kuonesha fursa mbalimbali zilizopo kwa wawekezaji nchini ikiwemo katika eneo la utafiti wa kina.

"Pamoja na kuendelea kukua kwa kasi kwa sekta yetu ya madini, Nchi yetu imefanikiwa kufanya utafiti wa kina kwa asilimia 16 pekee. Hivyo, iwapo tutaongeza eneo kubwa litakalokuwa limefanyiwa utafiti, kutatanua wigo wa taarifa zaidi za mashapo ya madini na kuvutia zaidi wawekezaji"

"Eneo hili la utafiti tunaona ni fursa kubwa ya kuanza nayo katika kuimarisha mashirikiano yetu na Serikali ya Urusi kutokana na hatua kubwa mliyopiga hususan katika utafiti wa kijiolojia na teknolojia ya kisasa kupitia maabara zenye vifaa bora" alisisitiza Mhe. Mavunde.

Aidha, Waziri Mavunde alimweleza Mhe. Naibu Waziri Tetenkin juu ya uwepo wa Hati ya Makubaliano(MoU) baina ya Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini (GST) na Chuo Kikuu cha Urusi ambayo bado haijakamilika na kumwomba kuiwekea nguvu ili ikamilike kwa wakati na kuanza utekelezaji ambao utasaidia kuimarisha ushirikiano kwenye utafiti baina ya Nchi zetu.

Katika hatua zingine, Mhe. Mavunde alieleza juu ya uhitaji wa kujengewa uwezo kwa wataalam katika eneo la utafiti wa jiolojia na maabara na kumuomba Mhe. Tetenkin kuona uwezekano wa kuimarisha ushirikiano zaidi katika eneo hilo ili wataalam wetu waweze kupata ujuzi na teknolojia vitakavyochochea maendeleo ya sekta ya madini.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Tetenkin aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kushirikiana kwenye nyanja mbalimbali za mashirikiano kiuchumi, na kueleza utayari wa Serikali ya Urusi katika kuimarisha ushirikiano huo.

Aidha, alisisitiza kuwa Urusi ipo tayari kuisaidia Tanzania katika eneo la utafiti wa kijiolojia na kuwajengea uwezo wataalam kutoka Tanzania na kushauri kuwa pamoja na MoU baina ya Taasisi zetu mbili, ni vyema ikaandaliwa MoU baina ya Serikali zetu kupitia Wizara za Madini itakayoonesha malengo yote tunayoitaji kuyatimiza kwa manufaa ya Nchi zetu. 

Katika hatia nyingine, Waziri Mavunde alifanya mazungumzo na *Bw. Sergey Chestnoy*, Mkurugenzi wa Idara ya Kimataifa wa Kampuni ya Rusal ambao ni wazalishaji wakubwa wa aluminum duniani na kuialika kampuni hiyo kufika Nchini Tanzania kwa lengo la kujadili juu ya uwekezaji katika utafiti wa kina na uchimbaji wa madini ya bauxite.



 

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3