*_MAKAMU WA RAIS AMWAKILISHA RAIS DKT. SAMIA SULUHU HASSAN KATIKA MAADHIMISHO YA SIKU YA MAZINGIRA DUNIANI*
Jun 5, 2026
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi ametoa wito wa kutumia Maadhimsho ya Siku ya Mazingira Duniani kukumbuka wajibu wa kuunganisha nguvu katika jitihada za kuhifadhi mazingira, na kuhakikisha matumizi adili ya rasilimali nyingi ambazo Tanzania imejaaliwa kuwa nazo.
Makamu wa Rais ametoa wito huo, alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani, ambayo Kitaifa yamefanyika katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete mkoani Dodoma.
Amesema baadhi ya mambo muhimu ya kuzingatia katika uhifadhi wa mazingira ni pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala ya mazingira na kuimarisha mfumo wa usimamizi wa taka hususan katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa dhana ya uchumi rejeshi, kwa kuwa maeneo mengi bado hali ya usafi haridhishi.
Makamu wa Rais ameongeza kwamba, ni vema kuendelea kubadili mtazamo ili kuziona taka kama fursa ya kiuchumi na kuzitumia kutengeneza bidhaa mbalimbali kama vile mbolea, chakula cha mifugo na bidhaa nyinginezo. Hali kadhalika, kuendelea kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ambapo hadi sasa, matumizi hayo yameendelea kuimarika kutoka 6.9% mwaka 2021 hadi kufikia 28.6% mwaka 2025.
Aidha, Makamu wa Rais amehimiza kuongezwa kwa jitihada za uhifadhi na utunzaji wa mazingira ambapo ameagiza Mamlaka zinazotoa vibali vya ujenzi kuweka sharti na kusimamia ili kila kibali cha ujenzi kinachotolewa kinaambatana na agizo la kupanda miti isiyopungua mitano pamoja na kuzielekeza Mamlaka za Serikali za Mitaa hususan Manispaa na Majiji kuazisha Bustani za kijani na kuhakikisha zinatunzwa ipasavyo.
Pia Makamu wa Rais ameagiza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania kuhakikisha uwepo wa miche ya miti ya kutosha ili kurahisisha na kuwezesha zoezi la upandaji miti nchini, Mamlaka husika kuimarisha udhibiti wa uharibifu wa maeneo yote yanayopandwa miti pamoja na kuiagiza Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia kituo cha Taifa cha kuratibu kaboni kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), kubainisha misitu inayofaa na kuisajili katika biashara ya kaboni.
Vilevile, Makamu wa Rais ametoa rai kwa Taasisi za utafiti kufanya tafiti kuhusu mimea au viumbe vamizi ambavyo vinazidi kuongezeka na kuathiri mifugo na mimea mingine katika maeneo mbalimbali nchini. Pia ameagiza Mamlaka za Serikali za Mitaa kuimarisha mifumo ya usimamizi wa taka hususan kuanzisha vituo vya kuchakata taka ili kupunguza kiasi cha taka katika madampo na kuchagiza urejelezaji.
Makamu wa Rais ametoa wito kwa kila mwananchi kuwajibika kuhakikisha kwamba suala la utunzaji na usafi wa mazingira, ikiwemo udhibiti wa taka linapewa kipaumbele. Amesema ni vema kutambua suala la ulinzi na uhifadhi wa mazingira halina mbadala, kwa kuwa mazingira ndiyo uhai na uchumi.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhandisi Hamad Masauni, amesema Uzinduzi wa Programu ya Mageuzi ya Kimkakati ya Mazingira Endelevu Tanzania, itakayotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano (2026 – 2030), imelenga kuchochea matokeo makubwa ya haraka katika kurejesha uoto wa asili, kuimarisha ustawi wa mfumo wa ikolojia pamoja na kutoa huduma za kiikolojia ambazo ni msingi muhimu wa uzalishaji katika sekta mbalimbali za uchumi.
Amesema hatua hizo zitaweza kuchangia katika kufanikisha malengo ya Dira 2050 ambayo inalenga kuifanya nchi kuwa na ustawi wa mazingira na ustamilivu mkubwa wa mabadiliko ya tabianchi. Ameongeza kwamba Programu hiyo, inalenga kuhamasisha upandaji wa miti bilioni mbili kila mwaka, kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia, kuimarisha usimamizi wa taka, kukuza biashara ya kaboni pamoja na kuongeza ushiriki wa wananchi hususani wanawake na vijana katika uchumi wa kijani.
Maadhimisho hayo, yaliobebwa na kauli mbiu isemayo, “Dira 2050: Tuwajibike Kukijanisha Tanzania” yamehudhuriwa na wadau mbalimbali wa mazingira wa Kitaifa na Kimataifa, Viongozi mbalimbali, Wanafunzi na Wananchi.



