Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
HALMASHAURI YA JIJI LA ARUSHA YATENGA FEDHA KWA AJILI YA UJENZI WA MIUNDOMBINU YA BARABARA.

HALMASHAURI YA JIJI LA ARUSHA YATENGA FEDHA KWA AJILI YA UJENZI WA MIUNDOMBINU YA BARABARA.

 

Na,Jusline Marco:Arusha

 Zaidi ya shilingi bilioni 3.7 za mapato ya ndani zimetengwa na Halmashauri ya Jiji la Arusha kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara, vivuko na mifereji ya maji ya mvua katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha miundombinu na kupunguza changamoto za usafiri hasa kipindi cha mvua za masika.


Akizungumza na waandishi wa habari, Mstahiki Meya wa Jiji la Arusha, Maximilian Iraghe, amesema fedha hizo ni kodi zinazolipwa na wananchi na zimelenga kutatua changamoto za muda mrefu za miundombinu katika kata mbalimbali za jiji hilo.


Amesema kati ya fedha hizo, kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 672 kimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa vivuko vikubwa (box culverts), vivuko vya kawaida pamoja na mifereji ya maji katika maeneo mbalimbali ikiwemo Kibo–Majengo hadi Mwimbo katika Kata ya Olasiti, pamoja na maeneo ya Shamsi, Kibanda Maziwa, Mto Rajabu na Oldonyo yaliyopo Kata ya Sombetini.

Meya Iraghe amesema mradi huo pia unahusisha uboreshaji wa barabara za Green Valley, Kirai, Oldonyo Kisimani, Pateli na Barbara katika kata za Ilboru na Sakina, ambapo kazi hizo zinatekelezwa na kampuni ya Grass Builders Limited ambayo tayari imeanza utekelezaji wa mradi huo.


Aidha, amesema kampuni ya Mandhaka Tanzania Limited imepewa kazi ya kujenga vivuko vikubwa na mifereji ya maji katika barabara za Banana, Isaababu na Safina zilizopo katika kata za Daraja Mbili na Kimandolu kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 585.


Katika hatua nyingine, kampuni ya Gianzhi Geo Engineering Group Corporation Limited inaendelea na ujenzi wa barabara ya Giriki kwa kiwango cha zege yenye urefu wa kilometa 1.1 kwa gharama ya takribani shilingi bilioni 1.8.


Meya huyo amewataka wananchi kufuatilia na kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo ili kuhakikisha thamani ya fedha inapatikana, akisisitiza kuwa fedha zinazotumika ni kodi zao na zinapaswa kuleta matokeo yanayoonekana.


Wakati huo huo, amesema Halmashauri ya Jiji la Arusha imetenga zaidi ya shilingi bilioni 7 kwa ajili ya sekta ya barabara katika mwaka mpya wa fedha unaoanza Julai mwaka huu, fedha ambazo zitaelekezwa katika ujenzi na ukarabati wa barabara za vumbi, vivuko na mifereji ya maji katika kata ambazo bado hazijafikiwa na miradi ya sasa.


Amesema hatua hiyo ni sehemu ya maandalizi ya kuboresha miundombinu ya jiji hilo kuelekea michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 pamoja na kuimarisha huduma za usafiri kwa wananchi wa Arusha.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3