WAANDISHI WA HABARI WATAKIWA KUTOA ELIMU KUEPUKA ATHARI ZA VURUGU
Na Matukio Daima Media
Waandishibwa habari nchini Tanzania wametakiwa kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu athari za maandamano yasiyo ya amani na vurugu, kwani matukio hayo yanaweza kuathiri maendeleo na rasilimali za taifa.
Rai hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam na Mwanafalsafa wa Pan-Afrika kutoka Zimbabwe, Dk. Joshua Maponga, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uzinduzi wa makala inayozungumzia matukio yaliyojitokeza kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Amesema kuwa, filamu hiyo inabainisha ushahidi unaothibitisha kuwa vurugu ziliratibiwa na kupangwa mapema ambapo wahusika waliongezwa na ushawishi kutoka nje ya nchi jambo ambalo halijawahi kuchapishwa katika vyombo vya habari vya kimataifa.
Ameongeza kuwa, hali hiyo ni hatari kwa ustawi na usalama wa taifa, hivyo akaishauri Serikali kuchukua hatua za kufanya uhakiki wa mashirika hayo ili kubaini vyanzo vya fedha wanazopata na namna zinavyotumika.
Aidha, ameeleza kuwa watu wanaochochea vurugu mara nyingi huishi nje ya nchi katika mazingira mazuri, huku wananchi wanaoshiriki machafuko hayo wakikabiliwa na madhara makubwa ikiwemo kupoteza maisha, mali na makazi yao.
Sambamba na hayo amewataka watanzania kuacha kusikiliza wanaharakati na wanasiasa wanaochochea vurugu na uvunjifu wa amani nchini, kwa kuwa watu hao hawana nia njema kwa taifa.
Dk. Maponga amesema kuwa baadhi ya mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) yamekuwa yakipokea fedha kutoka mataifa ya nje kwa lengo la kuhamasisha vitendo vinavyokwenda kinyume na maadili na amani ya nchi, ikiwemo vurugu na migawanyiko kati ya wananchi na viongozi wao.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa African Spear Head Media, David Hundeyin, amesema kuwa Tanzania ni moja ya nchi muhimu kiuchumi barani Afrika kutokana na nafasi yake ya kimkakati, hususani kupitia Bandari ya Dar es Salaam inayotumiwa na mataifa mbalimbali katika shughuli za biashara na uchumi.
Ameongeza kuwa, wananchi wanapaswa kulinda amani na rasilimali za nchi yao, kwani machafuko yanaweza kusababisha mdororo mkubwa wa uchumi na kuathiri maendeleo ya taifa.
"Vurugu na mauaji yaliyotokea Oktoba 29, 2025 yalikuwa na athari kubwa kwa jamii, hata hivyo, bado kuna baadhi ya watu wanaoendelea kutumia mitandao ya kijamii kuhamasisha vurugu, wananchi wanapaswa kuwa makini na watu wa aina hiyo kwa kuwa hawana nia njema kwa taifa lao,” amesema Hundeyin.
Makala hiyo imeandaliwa na kampuni ya African Spear Head Media, "Nini kilitokea octoba 29?" ambapo kutolewa kwa filam hiyo ni hatua muhimu kwa wanahabari na wazalishaji maudhui kiafrika wanaojitahidi kuhakikisha matukio tata ya kisiasa barani Afrika yanaripotiwa kwa usahihi na kwa kina.

