WANAFUNZI 16 WATEKETEA KWA MOTO NCHINI KENYA: TUNACHOJUA KUFIKIA SASA
Takriban wanafunzi 16 wamethibitishwa kufariki dunia kufuatia moto ulioteketeza bweni katika Chuo cha Wasichana Utumishi kilichopo Gilgil, Kaunti ya Nakuru, katika saa za mapema za Alhamisi.
Polisi wamesema wanafunzi wengine 74 wanapatiwa matibabu hospitalini baada ya kujeruhiwa katika tukio hilo.
Moto huo ulianza majira ya saa saba usiku (1:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki) na kuteketeza bweni la Meline Waithera lililokuwa na takriban wanafunzi 220, wakiwemo wa Kidato cha Pili, Kidato cha Tatu na Kidato cha Nne.
Ripoti ya polisi inaeleza kuwa mkuu wa shule aliarifu mamlaka majira ya saa kumi na nusu alfajiri (4:30 asubuhi), hatua iliyosababisha operesheni ya dharura kuanzishwa. Hata hivyo, Shirika la Msalaba Mwekundu Kenya limesema tukio hilo liliripotiwa mapema zaidi, takriban saa 3:30 usiku.
Timu za uokoaji zikiwemo wazima moto wa kaunti, maafisa wa polisi na wahudumu wa dharura zilifika eneo la tukio huku mamlaka zikianza oparesheni ya uokoaji, utafutaji na uhakiki wa idadi ya wanafunzi.
Naibu Mkuu wa Pili wa Jeshi la Polisi, Masoud Mwinyi, amesema uchunguzi bado unaendelea kubaini chanzo cha moto huo pamoja na ukubwa wa madhara yake, akionya dhidi ya uvumi wakati wataalamu wa uchunguzi wa kisayansi wakiendelea na kazi yao.
Ameeleza kuwa maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) pamoja na wataalamu wa uchunguzi wa kisayansi wamefika eneo la tukio.
“Timu za DCI na wataalamu wa forensiki tayari wapo eneo la tukio, na eneo limezingirwa.”
Ameongeza kuwa baadhi ya wanafunzi walikimbia kuelekea maeneo ya jirani wakati wa taharuki na bado wanatafutwa.
“Kwa sasa, maafisa wetu wanachunguza eneo kwa sababu baadhi ya wanafunzi walikimbia kwa hofu na mshtuko usiku.”
Mamlaka zinaendelea na zoezi la uhakiki wa majina ili kubaini idadi kamili ya wanafunzi wote waliokuwepo.
“Tunafanya kazi ya kuwatafuta wanafunzi wote na kufanya uhakiki kamili kuhakikisha kila mmoja anahesabiwa,” alisema Mwinyi.
Wazazi walijitokeza kwa wingi nje ya shule tangu asubuhi, wakiwa na wasiwasi mkubwa wakitafuta taarifa za watoto wao huku mlango wa shule ukibaki umefungwa kwa idadi kubwa ya watu.
Uongozi wa shule ulisema kuwa ni wazazi pekee ndio wataruhusiwa kuingia ndani kusaidia mchakato wa utambuzi na uhakiki wa wanafunzi.
Mashuhuda wamesema kulikuwa na hali ya taharuki kubwa wakati wanafunzi wakijaribu kutoroka kutoka katika jengo lililokuwa likiwaka moto.
Wambui Nderitu, ambaye mpwa wake ni mwanafunzi shuleni hapo, amesema alipokea simu muda mfupi baada ya moto kuanza.
“Niliambiwa saa nane usiku kuwa kuna moto, nikaitwa niende kuangalia mtoto wake,” amesema.
Nderitu amesema wazazi waliowasili shuleni walikuta hali ya taharuki na hofu kutokana na taarifa za vifo na majeruhi.
“Tulianza kufika mapema na tulipofika tulielekezwa kupanga foleni. Wengi tulikuwa na wasiwasi mkubwa kwa sababu tulikuwa tumesikia kuna waliokufa na wengine wamejeruhiwa na wako hospitalini.”
Amesema baadhi ya wanafunzi walijeruhiwa baada ya kuruka kutoka ghorofa ya juu wakijaribu kujiokoa.
“Baadhi waliokuwa ghorofa ya juu walilazimika kuruka, ndiyo maana wameumia.”
Nderitu ameeleza kuwa mpwa wake amenusurika moto huo lakini amevunjika mguu.
“Nilimkuta mpwa wangu… yuko salama… lakini amevunjika mguu,” alisema.
Kwa mujibu wa maelezo ya mpwa wake, moto huo huenda ulianza karibu na saa sita usiku.
Chanzo cha moto huo bado hakijabainika.
Mamlaka zimesema taarifa zaidi zitatolewa baada ya wanafunzi wote kuthibitishwa na uchunguzi kukamilika.