WAFANYABIASHARA WA RWANDA WALIA NA VIKWAZO VISIVYO VYA KIKODI
Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Serikali mkoani Kigoma imeahidi kutatua changamoto zisizo za kikodi zinazowakabili wafanyabiashara na wasafirishaji wa malighafi inayotumika kutengeneza Saruji (Clinker) kutokaCongo DR na kupitia Bandari ya Kigoma kusafirishwa kwenda nchini Rwanda.
Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma, Hassan Rugwa alitoa maelezo hayo baada ya kupokea ujumbe wa wafanyabiashara kutoka Rwanda wakiongozwa na Balozi wa Tanzania nchini Rwanda, Habib Kambanga wakiomba kufanyika kwa maboresho katika eneo la kuegesha magari, kupunguzwa kwa vizuizi vya barabarani pamoja na kuondolewa vikwazo visivyo vya kikodi.
Rugwa alisema kuwa baada ya kupokea maombi hayo amezielekeza Mamlaka husika kuchukua hatua za haraka kukabiliana na changamoto hizo ikiwemo kufanyika kwa maboresho ya eneo la Maegesho ya magari kwa kuweka miundombinu muhimu sambamba na kushughulikia vizuizi vilivyopo barabarani.
Awali Balozi Kambanga na alisema kuwa iwapo maboresho hayo yatafanyika kwa wakati, yataendelea kuimarisha mazingira ya biashara na usafirishaji katika ushoroba wa Kigoma na Rusumo mkoani Kagera kwani vikwazo hivyo kwa kiasi kikubwa vinapunguza kasi ya uzalishaji kutokana na malighafi hiyo kutofika viwandani kwa wakati.
Upande wake Meneja wa bandari za ziwa Tanganyika kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Edward Mabula, alisema kuwa wamepokea mapendekezo ya wadau hao na kuyafanyia kazi kwa kuangalia uwezekano wa kutenga na kujenga eneo la muda kwa ajili ya Maegesho ya magari hayo katika eneo la bandari ya nchi kavu Katosho iliyopo Manispaa ya Kigoma Ujiji.
Mwisho.
