META YAZINDUA MIPANGO YA USAJILI WA KULIPIA KWA FACEBOOK, INSTAGRAM NA WHATSAPP
Kampuni ya Meta imetangaza rasmi kuzindua mipango ya usajili wa kulipia kwa Facebook, Instagram na WhatsApp, hatua inayobadilisha kwa kiasi kikubwa namna kampuni hiyo itakavyopata mapato zaidi ya matangazo.
Mipango hiyo mipya ya “Plus” inaleta vipengele vya ziada kama filamu za hadithi za muda mfupi (Stories) zilizoongezwa muda wa kuonekana, kuongezwa kwa uonekano wa machapisho, ikoni maalumu za programu, stika za kipekee na uwezo wa kutazama hadithi bila kujitokeza kwenye orodha ya waliotazama.
Hatua hii inakuja wakati Meta inaongeza kwa kasi uwekezaji katika miundombinu ya akili unde (AI), ambapo inakadiriwa kutumia hadi dola bilioni 145 mwaka huu pekee kwa vituo vya data za AI na miundombinu husika.
Instagram Plus na Facebook Plus zitagharimu dola 3.99 kwa mwezi kila moja, huku WhatsApp Plus ikigharimu dola 2.99 kwa mwezi.
Meta imesema huduma hizi za usajili zinalenga watumiaji wanaotaka zana zaidi za kubinafsisha akaunti zao, kuongeza ushirikiano na hadhira, na kusimamia akaunti zao kwenye programu hizo.
Instagram Plus itakuwa na vipengele kama hesabu ya mara ambazo filamu za hadithi za muda mfupi (Instagram Stories) imetazamwa tena, orodha zisizo na kikomo za hadhira, muda mrefu wa kuonekana kwa Story zaidi ya saa 24, uangalizi wa siri wa Story, pamoja na kuangaziwa kwa filamu za hadithi za muda mfupi (Instagram Stories) kila wiki. Wateja pia watapata zana za kubinafsisha wasifu kama fonti maalumu, ikoni za programu, pini za ziada za wasifu na miitikio ya uhuishaji ya “Super Heart”.
Facebook Plus itakuwa na vipengele vinavyofanana, ikilenga zaidi ubinafsishaji wa wasifu na ushirikishwaji wa hadhira.
WhatsApp Plus inalenga zaidi ujumbe na ubinafsishaji, ambapo watumiaji watapata sauti maalumu za arifa, mandhari za programu, stika za hadhi ya juu, uwezo wa kubandika mazungumzo zaidi na zana za kupanga orodha za mawasiliano.
Mipango hiyo mipya ya Plus haitachukua nafasi ya Meta Verified, huduma ya sasa ya kulipia inayolenga uthibitisho wa utambulisho, ulinzi dhidi ya kujifanya mtu mwingine na huduma kwa wateja.
Wakati huo huo, kampuni hiyo inajaribu mpango mwingine wa usajili unaoitwa “Meta One” unaolenga watengenezaji wa maudhui, biashara na watumiaji wa Meta AI. Hatua hiyo inaifanya Meta kujiunga na kampuni kama Snapchat na X ambazo tayari zina huduma za usajili wa kulipia, ingawa mkakati wake unachanganya huduma za watumiaji, zana za wabunifu wa maudhui na huduma za AI katika mfumo mmoja mpana wa usajili.