Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
UAE YARIPOTI SHAMBULIO KARIBU NA KITUO CHA NISHATI YA NYUKLIA CHA ABU DHABI

UAE YARIPOTI SHAMBULIO KARIBU NA KITUO CHA NISHATI YA NYUKLIA CHA ABU DHABI

 

Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) imesema shambulio la droni lilisababisha moto karibu na kituo chake cha nishati ya nyuklia siku ya Jumapili, na kulielezea tukio hilo kama “ongezeko hatari la mzozo.”

Maafisa wanasema wanafanya uchunguzi kubaini chanzo cha shambulio hilo. Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo ilisema droni tatu zilivuka kuingia UAE kutoka “upande wa mpaka wa magharibi.”

Iliongeza kuwa droni mbili zilidunguliwa, lakini moja iligonga jenereta ya umeme “nje ya eneo la ndani la uzio wa usalama” wa Kituo cha Barakah kilichopo Abu Dhabi, na kusababisha moto.

Hakukuwa na majeruhi walioripotiwa, na pia hakukuwa na athari katika viwango vya usalama wa mionzi, mamlaka za eneo hilo zilisema.

Wizara ya Mambo ya Nje ya UAE ililaani shambulio hilo na kulielezea kama “kitendo kisichokubalika cha uchokozi,” ikisema ina haki ya kujibu vitendo vyovyote vya uhasama.

Pia iliongeza kuwa “kulenga vituo vya nishati ya nyuklia vya amani ni ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa, katiba ya Umoja wa Mataifa, na misingi ya sheria za kibinadamu.”

Wizara ya Ulinzi pia ilisema nchi hiyo “itakabiliana kwa nguvu dhidi ya majaribio yoyote ya kudhoofisha usalama wa taifa.”

Maafisa bado hawajasema droni hizo zilipotoka. UAE hapo awali imeishutumu Iran kuwa nyuma ya mashambulio dhidi ya miundombinu yake ya nishati na uchumi tangu vita vilipoanza katika eneo hilo mwezi Februari.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3